Shirika la Kutetea Haki za Binadamu
la Human Rights Watch limesema kuwa, waasi wa Tuareg pamoja na jeshi la
Mali wametenda jinai na ubaguzi dhidi ya raia wa makundi tofauti ya nchi
hiyo. Katika ripoti yake shirika hilo limesema kuwa, wanajeshi
wanawatesa Watuareg huku waasi nao wakiripotiwa kuwazingira na kuwapiga
mahasimu wao ambao wana ngozi nyeusi. Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa,
haki za binadamu za raia wa Mali zinakiukwa na askari jeshi wa nchi hiyo
na pia makundi ya waasi. Kwa sababu hiyo Human Rights Watch imezitaka
pande zinazopigana nchini Mali kuheshimu sheria za vita na kujiepusha na
kuwashambulia raia. Huko nyuma pia Shirika la Msamaha Duniani Amnesty
International lilisema kuwa, makundi yenye silaha hasa jeshi la Mali
ambalo lilikuwa likisaidiwa na vikosi vya Ufaransa yanakiuka haki za
binadamu, huku baadhi ya vitendo vikiweza hata kuitwa jinai za vita.
Mgogoro nchini Mali ulianza Machi mwaka
jana baada ya mapinduzi ya kijeshi, lakini ulishadidi na kupanuka baada
ya Ufaransa kushambulia kaskazini mwa nchi hiyo kwa kisingizio cha
kupambana na waasi.
No comments:
Post a Comment