Polisi nchini Tanzania wamemkamata mbunge wa Mtwara Mjini Hasnain
Murji kwa tuhuma za kuchochea vurugu za kupinga mradi wa bomba la gesi
kutoka mkoani humo kwenda mji mkuu wa nchi hiyo Dar es Salaam.
Msemaji wa Jeshi la polisi nchini Tanzania, Advera Senso amenukuliwa
na vyombo vya habari nchini Tanzania akisema kuwa Murji ambaye ni mbunge
wa chama tawala CCM alikamatwa nyumbani kwake maeneo ya Shangani mjini
Mtwara. Hivi karibuni pia viongozi wanne wa vyama vya upinzani mkoani
Mtwara walikamatwa na kufikishwa katika mahakama ya Mtwara Juni 4,
wakikabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama, kufanya uchochezi na
kuamsha hisia mbaya miongoni mwa Watanzania.
Murji amekamatwa ikiwa zimepita zaidi ya wiki mbili tangu kutokea
vurugu kubwa mkoani Mtwara. Ghasia hizo katika mkoa huo wa kusini
magharibi mwa Tanzania zilidumu kwa siku mbili, ambapo polisi
walipambana na makundi ya vijana wanaopinga mradi wa bomba la gesi
kujengwa. Watu kadhaa walipoteza maisha katika vurugu hizo na mali
nyingi kuharibiwa. Wakaazi wa Mtwara wanapinga wazo la kusafirishwa gesi
nje ya eneo hilo kwa njia ya bomba. Wanasema gesi inapaswa kusafishwa
katika eneo hilo kabla ya kusafirishwa ili wenyeji wapate ajira.
No comments:
Post a Comment