Wamisri waishio nje ya nchi leo wameendelea kupiga kura katika
uchaguzi wa rais ikiwa ni siku ya pili tokea zoezi hilo lianze siku ya
Alkhamisi. Kuna wagombea wawili tu katika uchaguzi wa rais nchini Misri
ambao wangali wanaendeleza kampeni zao huku wafuasi wa Harakati ya
Ikhwanul Muslimin wakisema uchaguzi huo ni kinyume cha sheria. Wamisri
waishio nje ya nchi wataendelea kupiga kura hadi kesho Jumamosi. Kuna
vituo 141 vya kupigia kura katika nchi 124 duniani ambapo Wamisri
wanaokadiriwa kushiriki katika zoezi hilo ni laki sita.
Kabla ya kuanza
zoezi la upigaji kura nje ya nchi, serikali iliondoa masharti magumu ya
wale wanaoweza kujisajili kwa ajili ya kupiga kura na ndio maana
inatazamiwa kuwa idadi ya wapiga kura itaongezeka. Uchaguzi wa rais
ndani ya Misri unatazamiwa kufanyika Mei 26 na 27 ambapo wagombea wawili
wanaowania kiti cha urais ni mkuu wa zamani wa jeshi Abdul Fattah
el-Sisi na mwanasiasa wa mrengo wa kushoto Hamdeen Sabahi. El-Sisi
ambaye alikuwa waziri wa ulinzi alikuwa na nafasi muhimu katika
kuondolewa madarakani Muhammad Morsi, rais aliyekuwa amechaguliwa kwa
njia halali. Morsi ni mwanachama mwandamizi wa Harakati ya Ikhwanul
Muslimin. Siku chache zilizopita katika kampenzi zake za uchaguzi,
el-Sisi alisema akichaguliwa atahakikisha kuwa Harakati ya Kiislamu ya
Ikhwanul Muslimin inafutwa kikamilifu katika medani ya kisiasa Misri.
Naye Hamdeen Sabahi amesema akichaguliwa atazingatia zaidi masuala ya
sera za kigeni ambapo amesisitizia ulazima wa kubadilisha vipengee vya
mkataba wa Camp David kati ya Misri na utawala wa Kizayuni na pia
kusitisha msaada wa kifedha wa Marekani kwa Misri. Huku hayo yakijiri
wapinzani wameshiriki katika maandamano dhidi ya serikali ya mpito na
zoezi zima la uchaguzi wa rais. Wafuasi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin
leo Ijumaa asubuhi wameandamana mbele ya Masjidul Istiqama katika
medani kuu ya mji wa Giza. Katika maandamano hayo wametoa nara dhidi ya
makamnada wa jeshi na polisi.
Waandamanaji na wapinzani wanaamini kuwa, uchaguzi wa sasa wa rais
nchini Misri si halali kwani Muhammad Morsi alipinduliwa baada ya kuwa
rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia Misri baada ya
kutimuliwa dikteta Hosni Mubarak. Wapinzani wanasema baada ya
kupinduliwa serikali halali ya Morsi, uchaguzi wa sasa wa rais ni hatua
ya jeshi kutwaa tena madaraka na kuirejesha Misri katika hali iliyokuwa
nayo kabla ya mapinduzi ya wananchi ya Februari 25 mwaka 2011.Ni kwa
sababu hiyo ndio maana 'Harakati ya Aprili 6' nayo pia ikajiunga na
wapinzani wanaosusia uchaguzi wa rais. Mratibu wa harakati hiyo, Amru
Ali amesema kile kinachojiri si uchaguzi bali ni zoezi la uteuzi wa
kumfanya Abdul Fattah el-Sisi awe rais wa Misri. Hali ya hivi sasa Misri
inaashiria ukweli huu kuwa, uchaguzi wa rais si tu hautasaidia
kurejesha utulivu nchini humo bali uchaguzi huo utazidisha ghasia na
machafuko katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
No comments:
Post a Comment