Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Tuesday, May 15, 2012

Mazungumzo yafanyika kati ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA

Mazungumzo ya siku ya kwanza   kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na ambayo hayakuhudhuriwa na vyombo vya habari yalifanyika jana alasiri huko mjini Vienna Austria.

Natija ya mazungumzo hayo yaliyodumu kwa muda wa saa tano na yaliyofanyika katika ofisi ya mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na karibu na ofisi ya Umoja wa Mataifa na ofisi nyingine za Kimataifa huko mjini Vienna, bado haijafahamika hadi sasa.
Mazungumzo hayo yameendelea hii leo kwa kuhudhuriwa na Ali Asghar Sultaniye Mjumbe wa kudumu wa Iran katika wakala huo na Herman Nackaerts Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IAEA.
Katika hali hiyo viongozi wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wa IAEA wamefafanua kuwa, wameamua kukaa katika meza ya mazungumzo kutokana na kuwepo mitizamo chanya ya kufikiwa maelewano kati ya pande mbili hizo.
Hali hiyo inaonyesha nafasi nzuri ya uwezekano wa kufikiwa maelewano yenye lengo la kutatua sutafahumu ambayo imekuwepo kwa muda mrefu kati ya pande mbili kuhusiana na mpango wa nyuklia wa Iran. Hata hivyo hii si mara ya kwanza kwa pande hizo kukaa katika meza moja ya mazungumzo. Nukta hiyo inaunga mkono ukweli kwamba, sasa pande mbili zimeazimia kutatua matatizo yaliyopo na kuimarisha ushirikiano wao kupitia mazungumzo, hali ambayo imezifanya baadhi ya nchi za Magharibi kuhaha huku na kule ili kuvuruga ushirikiano huo. Kuendelea na siasa zilizokwama za vikwazo visivyo vya kisheria na visivyofuata mantiki dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa siasa za kijuba za Wagharibi. Suala muhimu hapa ni kwamba, mazungumzo hayo yenye uonekano chanya kati ya Tehran na IAEA yanafanyika katika kipindi cha kukaribia duru ya pili ya mazungumzo ya pande mbili yanayotarajiwa kufanyika wiki ijayo baina ya kundi la 5+1 yaani Marekani, Uingereza, Ufaransa, China, Urusi na Ujerumani na Iran mjini Baghdad Iraq. Kwa ibara nyingine ni kuwa, mazungumzo hayo ya Baghdad ni natija ya maelewano yaliyofikiwa katika kikao cha mjini Istanbul Uturuki kati ya pande mbili hizo yaani kati ya kundi la 5+1 na Tehran.
Kuna nukta mbili muhimu ambazo zinaweza kuyafanya mazungumzo kati ya Iran na IAEA kuwa yenye natija nzuri na ya kimantiki. Nukta ya kwanza ni uwazi wa wakala huo kwa Tehran katika fremu ya ushirikiano wa Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezwaji wa Silaha za Nyuklia NPT. Aidha ni vyema kukumbusha hapa kwamba, kwa mara kadhaa Iran imetoa nafasi kwa wakurugenzi wa IAEA kutembelea kituo chake cha kijeshi cha Parchin kilichoko mashariki mwa Tehran, suala linaloonesha kwamba, shughuli za nyuklia za Iran zinafanyika kwa uwazi, malengo ya amani na kwa ushirikiano na wakala huo.
Ama nukta ya pili ni kuthibitishiwa Iran nia njema na uaminifu wa upande wa pili kuhusiana na shughuli zake za nyuklia. Hii ni kwa sababu kupuuzwa jambo hilo na nchi za Magharibi huko nyuma kumepelekea kutolewa ripoti zisizo na msingi na IAEA kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran. Ni wazi kuwa iwapo nukta mbili hizo zitazingatiwa na pande husika, tunaweza kuwa na matumaini kuwa mazungumzo yajayo yatakuwa na natija nzuri kwa pande zote mbili. 

No comments: