Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Sunday, April 29, 2012

Zimamoto wavuna mamilioni kwa kuuza stika bandia

Na Omary Kisimba, Mwanza
KIKOSI cha Zimamoto nchini kimeingia katika kashfa ya ufisadi mkubwa baada ya baadhi ya watumishi wake nchini kudaiwa kuunda mtandao wa kuuza stika bandia za ukaguzi wa vifaa vya kuzimia moto kwenye magari na kujiingizia mamilioni ya fedha kinyume cha sheria.

Stika halisi za zimamoto hutolewa na Idara hiyo kwa magari mbalimbali lakini baadhi ya watumishi wakisghirikiana baadhi ya vigogo wa taasisi hiyo, wamesuka mtandao ambao wamefanikiwa kutengeneza stika hizo bandia na kuziuza bila hata kufanya ukaguzi kwenye magari ambayo watayakamata yakiwa hayana vifaa vya zima moto.

Kutokana na kushamiri kwa hali hiyo, Mwananchi Jumapili lilifanya uchunguzi katika Jiji la Mwanza kwa kutumia magari mawili aina ya Canter na Scania ambayo hayakuwa na vifaa vya zima moto na hayakuwa yamekaguliwa na walipatiwa stika hizo bandia bila kugaguliwa kutoka kwa maofisa hao kwa bei ya Sh20,000 na Sh30,000.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa stika bandia hudurufiwa kitalaamu kwa kutumia kompyuta ambapo namba zake zinaonekana kuchapwa kwa kompyuta tofauti na zile halisi ambazo zimechapwa kwa mashine maalumu.
Pia stika hizo bandia hazina viwango kamili vya bei na wateja wanapouziwa na watumishi hao wa Zimamoto huwa hawapewi stakabadhi ya manunuzi.


Uchunguzi huo uliofanywa kwa muda mrefu, umebaini kuwa stika hizo zimekuwa zikiuzwa na maofisa hao wa Zimamoto na zaidi, nyingi zimekuzwa kwa mgari ya watu binafsi na mashirika binafsi na magari ya abiria hususan daladala.

Mmoja wa maofisa wa Zimamoto jijini Mwanza ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alikiri kuwepo kwa mtandao huo na kuongeza: “Ukiona hapa ofisini kwetu ni kuwa kila ofisa anakitabu chake, jambo hili lipo karibu kila mkoa mkifuatilia mtalikuta na kila ofisa analetewa na ofisa wake toka makao makuu na wengine baada ya kuziuza kwa muda mrefu, wameanza kutengeneza za kwao.”


Alisema kwa wiki huuzwa stika zaidi ya 10 hadi 20 na kuongeza kuwa wakati wa ukaguzi wa magari, mauzo huwa makubwa kwani stika hununuliwa kama njugu na wamekuwa wakiuza stika zao binafsi na zile za Serikali huuzwa baadaye.


Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto Mwanza, ACP Julius Bulambo alipoulizwa kwa njia ya simu jana, alisema hayuko tayari kuzungumzia jambo hilo na kukata simu, alipopigiwa tena, simu yake iliita bila majibu.

Kwa upande wake, Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto Makao Makuu, jijini Dar es Salaam, Marko Shija, alikiri kuwepo kwa wizi huo na kuongeza kuwa vitendo hivyo hufanywa na watu wasio waaminifu.

Hata hivyo hakuwa tayari kueleza ni hatua zipi ambazo mpaka sasa Kikosi hicho kimechukua na kumtaka mwandishi kuwasiliana na Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto Mwanza ambaye hakupokea simu.

No comments: