Rais Jakaya Kikwete wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema, nchi yake haina tatizo na muungano wa kisiasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilimradi muungano huo uanzishwe baada ya kukamilishwa kwa hatua nyingine zote muhimu za ushirikiano baina ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Rais Kikwete amesema Tanzania haiwezi kuwa na tatizo na Muungano huo kwa sababu Taifa la Tanzania lenyewe ni matokeo ya muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar na ina uzoefu na muungano wa kisiasa. Hayo yanajiri katika hali ambayo, hatua za kufikia muungano wa kisiasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekuwa za kusuasua mno kutokana na kuweko baadhi ya hitilafu baina ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Tanzania imekuwa ikionyeshewa kidole cha lawama kutokana na kile kinachoonekana kama ukwamishaji wa baadhi ya mambo unaofanywa na nchi hiyo. Hata hivyo, viongozi wa Dar es Salaam wamekuwa wakisisitiza juu ya kufanywa mambo kwa umakini kuelekea katika muungano na hivyo kuweka kando hatua za pupa.
No comments:
Post a Comment