Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Sunday, February 8, 2015

Wanajeshi 8,700 kukabiliana na Boko Haram

Nigeria na nchi jirani  zimeahidi kuunda kikosi cha askari 8,700 kukabiliana na kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo limeeneza ugaidi nje ya mipaka ya nchi hiyo. Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi baada ya kikao cha siku tatu huko Yaounde mji mkuu wa Cameroon, wawakilishi wa Benin, Cameroon, Niger, Nigeria na Chad wameafiki kuunda kikosi cha askari 8,700 kwa lengo la kukabiliana na Boko Haram.
Kufuatia uamuzi huo, Umoja wa Afrika unatazamiwa kuwasilisha mpango wa kikosi hicho kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuidhinishwa rasmi. Kundi hilo la kitakfiri limeua watu zaidi ya 13,000 na kupelekea wengine takribani milioni moja na nusu kuachwa bila makao tokea mwaka 2008.
Tayari wanajeshi wa Chad na Niger wameshatuma wanajeshi wao Nigeria kukabiliana na magaidi wa Boko Haram.
Duru za usalama zinadokeza kuwa kundi la Boko Haram lina magaidi sugu karibu elfu sita. Huku hayo yakijiri Tume ya Uchaguzi Nigeria imetangaza kuakhirisha uchaguzi wa rais na bunge uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 14. Uchaguzi huo umeakhirishwa hadi Machi 28 kwa ajili wanajeshi wanaopambana na Boko Haram hawawezi kudhamini usalama wa wapigaji kura kwa sasa.

No comments: