Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Wednesday, May 23, 2012

Ajali yaua tisa, wamo waombolezaji

Waandishi Wetu; Victor Mongi
WATU tisa wamefariki dunia na wengine 20 kujeruhi kwenye ajali ya gari katika matukio mawili yaliyotokea wilaya za Babati, mkoani Manyara na Kilosa Morogoro.

Taarifa zilidai kuwa wakati watu watano wakifariki dunia na tisa kujeruhiwa wilayani Babati, wengine wanne walifariki duni na kumi kujeruhi katika ajali ya gari aina ya Fuso, wilayani Kilosa.
Ajali iliyoua watu watano mkoani Manyara, ilitokea baada ya gari walilokuwa wamepanda kupinduka mara kadhaa kwenye barabara ya Halla Galapo, Wilaya ya Babati, mkoani Manyara.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Manyara, Eurelia Msindai, alisema ajali hiyo ilitokea juzi eneo la Halla Galapo na kwamba, watu hao walikuwa wakitoka msibani.

Msindai alisema wote ni wakazi wa Kata ya Mamire, walipata ajali wakiwa wamepakia kwenye gari aina ya Toyota Lucida.

“Chanzo cha ajali hiyo ni kifaa kijulikanacho kama excel ya nyuma ya upande wa kushoto ya gari hilo kukatika na gari kupoteza mwelekeo na kupinduka mara kadhaa zaidi ya mita 70,” alisema.
Alisema watu wanne walikufa papo hapo na mmoja alifia hospitalini na kwamba, majeruhi sita wamelazwa hospitalini hapo na watatu wamepelekwa Hospitali ya Rufani KCMC Moshi.
Katika tukio lingine, watu wanne wanadaiwa kufa na zaidi ya 10 kujeruhiwa baada ya gari aina Fuso lililokuwa limepakia mizigo na abiria kupinduka eneo la Kwambe Dumila -Njia Tatu, barabara ya Morogoro – Dodoma.

Ofisa Tarafa wa Magole, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro, Conlard Mzwalandili, aliwataja watu waliokufa katika ajali hiyo juzi kuwa, ni wanawake wawili na wanaume ambao wote ni wajasiriamali wa Dumila.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Spola Martin Leonard (30), Noadia Keneth (33), Hemed Stadi (40) na Mohamed Seif Angoo (33) na kwamba, majeruhi walipelekwa Hospitali ya Roma iliyopo Mji mdogo wa Dumila, baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Rufani Mkoa wa Morogoro.

Mzwalandili alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 10:00 jioni na kwamba, taarifa za awali zinadai ilitokana na kubeba mizigo na abiria kuliko uwezo wake ikiwamo mwendokasi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Adolophina Chialo, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kwamba, watu wawili walikufa na 11 kujeruhiwa, huku dereva wa gari hilo alikilimbilia.
Imeandikwa na Joseph Lyimo, Babati na Esther Mwimbula, Kilosa

No comments: