Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Tuesday, June 3, 2014

Rais mpya wa Malawi ataka uwepo uthabiti wa uchumi

Rais Peter Mutharika wa Malawi amesema kuwa, sera za serikali yake zitajikita zaidi katika kuleta uthabiti wa kiuchumi na umoja wa kitaifa nchini humo. Akizungumza mara baada ya kuapishwa rasmi jana kuwa Rais wa Malawi, Peter Mutharika ameongeza kuwa uchumi wa nchi hiyo utastawi hadi kufikia asilimia saba kwa mwaka. Rais Peter Mutharika ni ndugu wa Bingu wa Mutharika Rais wa zamani wa nchi hiyo aliyefariki dunia Aprili 2012 na nafasi yake kuchukuliwa na Makamu wake Joyce Banda ambaye alishindwa vibaya kwenye uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 20 mwezi uliopita.
Joyce Banda alifeli katika juhudi zake za  kuboresha hali ya uchumi, uhaba wa nishati na hasa mafuta na kuzuia kuporomoka sarafu ya nchi hiyo. Mfuko wa Kimataifa wa Fedha IMF umeeleza kuwa, tokea Joyce Banda aliposhika madaraka ya nchi hiyo mwaka 2012, thamani ya sarafu ya nchi hiyo ilizidi kuporomoka na bei za bidhaa mbalimbali kupanda maradufu. Mashirika ya kifedha duniani pamoja na nchi wahisani zilisimamisha kutoa misaada ya kifedha kwa Malawi baada ya kufichuliwa kashfa ya ufisadi wa mamilioni ya dola katika serikali ya Joyce Banda. Inafaa kuashiria hapa kuwa, Rais Peter Mutharika aliapishwa rasmi jana mjini Blantyre, kwenye sherehe ambazo zilisusiwa na washindani wake kwenye uchaguzi huo ambao ni Bwana Lazarus Chakwera wa Malawi Congress Party na Joyce Banda Rais aliyeondoka madarakani.

No comments: