Kufuatia kuvunjika mazungumzo ya kitaifa kati ya makundi ya kisiasa kwa
lengo la kufikiwa makubalino ya kitaifa nchini Yemen, hapo jana Ijumaa
tume ya mapinduzi sanjari na kuitisha kongamano lililoyahusisha makundi
tofauti ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kielimu, ilitangaza katiba mpya
ya mpito ambayo inatazamiwa kumaliza hali ya mchafukoge nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa ya ikulu ya rais mjini Sana’a iliyotangazwa
kupitia televisheni ya taifa, katiba hiyo ya mpito, inajumuisha kuundwa
baraza la rais wa nchi na baraza la kitaifa kwa minajili ya kumaliza
mgogoro wa taifa hilo.
Mawazi wa Mambo ya Ndani na Ulinzi na hali
kadhalika viongozi wa idara ya usalama, ni miongoni mwa waliohudhuria
kikao hicho katika ikulu ya rais. Katiba hiyo ya mpito na baraza la rais
nchini Yemen, vitaliongoza taifa hilo kwa kipindi cha miezi mitatu toka
sasa. Kabla ya hapo na katika mazungumzo yaliyofanyika mjini Sana’a
makundi ya kisiasa, yalikubaliana, kuunda baraza la rais lenye shakhsia
watano ambalo litakuwa chini ya Ali Nasir Muhammad rais wa zaman wa
Yemen ya Kusini kabla ya nchi hiyo kuungana na ya Kaskazini hapo mwaka
1990. Kabla ya hapo yaani siku ya Alkhamis iliyopita tume hiyo ya
mapinduzi ilikuwa imetangaza kuwa, kufuatia kuvunjika mazungumzo ya
kisiasa ingetangaza katiba ya mpito chini ya usimamizi wa Jamal Benomar,
mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini humo. Kwingineko duru za
habari zimeripoti kuwasili Benomar, nchini Saudia kabla ya kutangazwa
katiba hiyo. Huku hayo yakijiri, tume ya mapinduzi nchini humo,
imetangza kuvunjwa kwa baraza la wawakilishi na badala yake kuundwa
baraza la mpito linalowajumuisha wabunge 551. Mmoja wa wawakilishi wa
tume ya wananchi amenukuliwa akisema kuwa, kutangazwa katiba mpya nchini
Yemen, kumeonyesha matunda ya kikao cha mapinduzi na kuongeza kwamba,
katiba hiyo ni kwa madhumuni ya kufikiwa uhuru na utukufu wa Wayemen
wote. Ameongeza kuwa, mapinduzi ya wananchi hayakuwa bila faida na
kwamba, wananchi wote wa taifa hilo wanapasa kujitolea kwa ajili ya
kuisafisha nchi yao kutokana na mafisadi sanjari na kuwafikisha mbele ya
vyombo vya sheria, hasa kwa kutilia maanani kwamba lengo la mapinduzi
hayo lilikuwa ni kuleta marekebisho nchini humo. Muhammad al-Bakhiti,
mwakilishi wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Answarullah nchini Yemen,
ameitaja pia katiba hiyo kuwa njia ya kutatuliwa mgogoro wa kisiasa
nchini humo na kusisitiza kuwa, chama cha mrengo wa marekebisho chenye
mafungamano na kundi la Ikhwanul Muslimin na baadhi ya makundi mengine,
ndio chanzo cha kufeli mazungumzo ya kisiasa nchini, hasa kutokana na
mirengi hiyo kufuata amri kutoka nje. Inatazamiwa kuwa, kutangazwa
katiba ya mpito nchini Yemen, kutaweza kuhitimisha mgogoro wa kisiasa
nchini humo sanjari na kufanikisha kuundwa serikali ya wananchi
itakayozijumuisha shakhsia mbalimbali na kuundwa Yemen moja yenye nguvu
na iliyo na shikamano imara wa kitaifa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment