Maafisa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo juzi Alkhamisi
walitangaza habari ya kutokea mapigano kati ya askari jeshi wa nchi hiyo
na Rwanda katika mpaka wa pamoja wa nchi hizo jirani. Walisema mapigano
hayo yalipelekea kuuawa kwa askari watano wa Kongo. Mapigano mengine
kama hayo yaliyojiri siku ya Jumatano yalipelekea askari wengine kadhaa
kuuawa na kujeruhiwa. Maafisa wa nchi hizo wamekuwa wakituhumiana na
kunyoosheana vidole kuhusiana na msababishaji hasa wa kuongezeka mvutano
katika mpaka wao wa pamoja.
Julien Kahongya Paluku, Gavana wa Jimbo la
Goma, makao makuu ya Kivu Kaskazini, mashariki kwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo amewatuhumu askari wa Rwanda kuwa ndio walioanza
kuwafyatulia risasi wenzao wa Kongo, na kuongeza kuwa askari wa Kongo
wametakiwa kujizuia kujibu mashambulio ya askari wa Rwanda kadiri
wanavyoweza.
Kwa upande wao maafisa wa Rwanda wanasema kuwa mashambulio ya askari
wa DRC katika ardhi yao ni jambo la kawaida na kuwa huwa wanavuka mpaka
na kuingia katika ardhi ya Rwanda kwa lengo la kuwinda wanyama wa
porini. Hata hivyo wanasema katika matukio ya hivi karibuni
hawakuwafyatulia risasi wanyama tu bali waliwafyatulia pia risasi askari
wa Rwanda. Wakazi wa miji ya mpakani ya Rwanda pia wamesema kuwa askari
hao wa Kongo walianza kufyatuliana risasi na askari wa Rwanda
walipoingia katika ardhi ya nchi hiyo kwa lengo la kuiba mifugo.
Akizungumzia mapigano hayo, Martin Kobler, mkuu wa kikosi cha kulinda
amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
amezitaka pande mbili hizo kuwa na subira na kufanya juhudi za kurejesha
amani na utulivu katika mpaka wao wa pamoja. Maafisa wa kimataifa
wanatumai kwamba pande mbili hizo zitaheshimu na kutekeleza kikamilifu
Mkataba wa Amani, Usalama na Ushirikiano katika eneo la Maziwa Makuu
uliotiwa saini tarehe 24 Februari mwaka uliopita huko Addis Ababa
Ethiopia.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa chanzo hasa cha mapigano
na mivutano katika mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda
ni uungaji mkono wa Kongo kwa waasi wa FDLR wa Rwanda ambao wana kambi
zao katika ardhi ya nchi hiyo. Waasi hao ambao ni wa kabila la Hutu
wanatuhumiwa na serikali ya Kigali kwamba wanafanya njama za kuzusha
ghasia na machafuko huko Rwanda. Waasi hao walihusika pakubwa katika
mauaji ya kimbari ya 1994 nchini Rwanda, mauaji ambayo yalidumu kwa muda
wa zaidi ya miezi mitatu na kupelekea watu laki nane kupoteza maisha
yao. Hii ni katika hali ambayo wajuzi wengine wa mambo wanasema kuwa
mapigano ya hivi karibuni yamechochewa na Rwanda kwa lengo la kulinda
maslahi yake katika eneo hilo. Nchi hiyo imekuwa ikituhumiwa na Umoja wa
Mataifa kwamba inawapa silaha waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
kwa lengo la kupora madini ya nchi hiyo. Rwanda na Uganda zimekuwa
zikituhumiwa kuingilia mambo ya ndani ya Kongo kwa sababu mbalimbali na
hasa ya kupora maliasili za nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment