Rais Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania juzi Alkhamisi, aliwatuhumu
wapinzani wa serikali yake kuwa wanafanya njama za kuzusha machafuko
ndani ya nchi hiyo. Katika wiki za hivi karibuni, wapinzani wamekuwa
wakifanya maandamano ya mara kwa mara sambamba na kutoa nara dhidi ya
serikali ya Nouakchott na kutaka kususiwa uchaguzi ujao wa rais
uliopangwa kufanyika tarehe 21 ya mwezi huu wa Juni. Hii ni katika hali
ambayo vyama vya upinzani, sanjari na kuhoji juu ya uhalali na mwenendo
wa uchaguzi huo, vimekituhumu chama tawala kwa kufanya njama za kuiba na
kubadili matokeo ya uchaguzi huo.
Makundi ya upinzani yanasema hatua ya
kutangazwa tarehe ya uchaguzi na upande mmoja tu ni njama ya serikali
ya kutaka kufanya uchakachuaji katika uchaguzi. Wakati huo huo, Rais
Ould Abdel Aziz amesema njama za wapinzani za kutaka kuingia madarakani
kwa nguvu zitaambulia patupu. Rais Ould aliyasema hayo katika mkutano
mmoja wa kampeni za uchaguzi mjini Nouakchott. Aidha rais huyo sambamba
na kuwatuhumu wapinzani kwa uongo, amesema watu wanaopanga kususia
uchaguzi kuwa ni mabaki ya utawala mbovu uliopita na kuwataka wafuasi
wake wahudhurie kwa wingi katika uchaguzi huo. Ould Abdel Aziz ambaye
pia ni jenerali wa zamani wa jeshi, atachuana na wagombea wanne akiwemo
mwanamke mmoja katika kutetea kiti chake cha urais. Kuna wasi wasi
kwamba, uchaguzi huo huenda ukavuruga hali ya mambo nchini Mauritania.
Jumuiya ya Kidemokrasia na Umoja ambao ni muungano wa wapinzani nchini
humo, sambamba na kutoa tamko imetangaza kuwa, hakuna dhamana yoyote
inayohakikisha kuwa uchaguzi huo wa rais utafanyika kwa uhuru na haki au
kuufanya uonekane kuwa na itibari. Ni kwa ajili hiyo ndio maana
muungano huo, ukayataka makundi mengine kususia uchaguzi huo. Mbali na
hayo wapinzani pia wametangaza azma yao ya kufungamana na mazungumzo na
serikali. Hata hivyo wamedai kuwa, viongozi wa chama tawala hawako jaddi
kuendelea na mazungumzo kwa lengo la kuukwamua mzozo wa nchi hiyo. Rais
Mohamed Ould Abdel Aziz ambaye aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya
kijeshi, sanjari na kuitisha uchaguzi wa mwaka 2009, amejitahidi
kuhakikisha utawala wake unatambuliwa kisheria. Hii ni katika hali
ambayo wapinzani wa Mauritania wanaitaja hatua hiyo kuwa ni hila kwa
ajili ya kupora madaraka ya taifa hilo. Kwa miaka yote ya hivi karibuni,
utawala wa Rais Ould Abdel Aziz umekuwa ukishuhudia maandamano na
malalamiko ya wananchi. Vitendo vya udikteta na kuwekewa mibinyo watu
maalumu kwa upande mmoja na kadhalika kushindwa kuimarisha hali ya
usalama nchini kwa upande mwingine, kumepunguza uungaji mkono wa
wananachi kwa rais huyo. Vitendo vya kigaidi katika miaka iliyopita, ni
jambo jingine ambalo limeathiri usalama wa taifa hilo. Mbali na suala la
usalama, kukosekana ridhaa ya kisiasa nchini Mauritania, umasikini na
ubaguzi uliokita mizizi, ni mambo mengine ambayo yamezusha hali ya
mchafukoge ndani ya nchi hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment