Kiongozi wa chama cha upinzani RENAMO nchini Msumbiji, Bwana Afonso
Dhlakama, ameitaka serikali ya nchi hiyo kuandaa mazingira mazuri ya
kufanyika uchaguzi mkuu. Dhlakama ameyasema hayo jana huku akiikosoa
serikali ya Maputo kwa kukwamisha mwenendo wa uchaguzi na kuanza kampeni
za uchaguzi huo mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 15 Oktoba mwaka huu.
Afonso amesema kuwa, ili aweze kushiriki katika uchaguzi huo, serikali
ya Rais Armando Guebuza wa nchi hiyo, inatakiwa kwanza imdhaminie
usalama wa kutosha wa kuendesha kampeni zake katika maeneo tofauti ya
nchi.
RENAMO ni chama kikubwa chenye wawakilishi wengi bungeni nchini
Msumbiji, huku ukiwa na viti 51 kati ya viti vyote 250 bungeni. Chama
hicho kilitia saini makubaliano ya usitishaji vita mwaka 1992. Hata
hivyo ilianzisha mashambulizi yake dhidi ya serikali hapo mwaka jana kwa
madai kwamba serikali ya Rais Guebuza haikutekeleza uadilifu katika
ugawaji wa mali za taifa hilo. Mwezi uliopita chama hicho kilisaini
makubaliano ya awali na serikali ya Maputo ambapo kwa mujibu wa
makubaliano hayo, waasi hao wa RENAMO watajiunga katika jeshi na polisi
ya nchi hiyo. Hata hivyo ilisisitiza kuwa, hawataweka chini silaha hadi
pale kutakapotiwa saini makubaliano ya mwisho na serikali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment