Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (CCM), kwa mara nyingine
ameingia katika kashfa nzito akituhumiwa kutaka kumpiga Mbunge wa Viti
Maalumu CUF, Moza Abeid ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Tukio hilo lilitokea mwanzoni mwa wiki ambapo
imeelezwa kuwa Nkamia mbali na kutaka kumpiga mbunge huyo, pia alimtolea
matusi mazito ya nguon. Kwa mara ya kwanza mbunge huyo aliingia katika
kashfa baada ya kutoa kauli bungeni kuwa hazungumzi na mbwa, bali
anazungumza na mwenye mbwa kabla ya kuingia katika mzozo na wahariri na
baraza la habari aliposema kuwa Jukwaa la Wahariri na Baraza la Habari
ni NGOs za kutafuta fedha.
Uchunguzi ambao umethibitishwa na
Nkamia mwenyewe umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni kutokana na
kuzomewa kwa Nkamia katika kampeni za uchaguzi mdogo Kata ya Dalai
Wilaya ya Chemba.
Kwa mujibu wa wabunge mashuhuda ambao waliliona
tukio hilo, ilielezwa kuwa Nkamia, ambaye pia ni mwandishi wa habari,
alianza kumshushia matusi Moza wakiwa ndani ya Bunge hadi walipotoka nje
alimfuata na kutaka kumpiga.
“Kweli pale jamaa yetu, alitia aibu, hata hivyo
kusema kuwa alikuwa amelewa siyo kweli maana mimi namfahamu Nkamia
vizuri ila ilikuwa ni hasira tu,” alisema mmoja wa wabunge walioamua
ugomvi huo.
Akizungumzia tukio hilo Moza, alisema kuwa wakati
akitoka nje ya ukumbi, alipita karibu na kiti anachokaa Nkamia na ghafla
akaitwa, lakini akashangazwa na kitendo cha kuanza kurushiwa matusi.
“Kweli Nkamia na mimi tunatoka wilaya moja, lakini
siku ile nilishangaa alinitukana matusi ya nguoni kabisa ………
(anayataja), lakini mimi kule sikusema kitu hadi nilipotoka nje
alinifuata na mimi hasira ilinishika nikaanza kumjibu akatupa vitabu ili
aje anipige wabunge wenzake wakamkamata,” alisema Moza.
Alisema kuwa chanzo cha matusi hayo ilikuwa ni
tuhuma kwamba Nkamia alimtuhumu Moza kuwa aliandaa vijana katika Kata ya
Dalai wakati wa kampeni za uchaguzi wa udiwani ili wamtukane.
“Hata hivyo, waliomwambia hivyo kwamba niliandaa
vijana au nilimtukana walimdanganya kwani mimi wakati huo nilikuwa
bungeni, lakini yeye ndiye aliyeniporomoshea matusi katika kampeni hizo
na ushahidi wa sauti ninao,” alisisitiza Moza.
Kwa upande wake Nkamia, ambaye kabla ya kuwa
mbunge alikuwa mtumishi wa Serikali katika Shirika la Tanzania
Broadcasting Corporation (TBC) alikiri kutokea kwa tukio hilo, lakini
alikanusha kuingia bungeni akiwa amelewa kama ilivyoaminika na watu.
Nkamia alitoa sababu za ugomvi huo kuwa ni
kutokana na taarifa kuwa Moza aliandaa kikosi cha vijana wahuni
kulishambulia gari la Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kuwazomea
viongozi wake akiwemo yeye.
“Ile ilikuwa ni hali ya kawaida kwa binadamu kupatwa na hasira
unapoambiwa kitu kama hicho, lakini sina shida na mbunge Moza na wala
sioni kama hilo ni tukio kubwa kiasi cha kuandikwa,” alisema Nkamia.
Mbunge Machali, apigwa alazwa hospitali
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kasulu Mjini,
Moses Machali (NCCR-Mageuzi), amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
wa Dodoma baada ya kupigwa na watu wasiojulikana wakati akitoka
kuhudhuria vikao vya Bunge juzi.
Tukio la kuvamiwa na kupigwa kwa mbunge huyo,
lilitokea saa 2.30 usiku wakati akirejea nyumbani kwake eneo la Area ‘E’
karibu na hoteli maarufu ya Summit.
Kwa mujibu wa Machali, watu hao ambao idadi yao
haikujulikana, walimsimamisha akiwa mita chache kabla ya kuingia
nyumbani kwake akiwa na gari yake ndipo wakaanza kumrushia maneno makali
na kumtaka ashuke ndani ya gari.
“Sikuweza kuwafahamu na idadi yao sikuipata mara
moja, lakini wameniumiza sehemu mbalimbali za mwili na hasa katika mguu
wangu wa kulia sehemu ya paja na sehemu ya pua kama mnavyoona,”alisema
Machali.
Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa Chama cha
NCCR –Mageuzi James Mbatia, alisema ni tukio baya na ambalo limeonyesha
kulikuwa na makusudi maalumu ya kufanya hivyo.
“Ni mapema kueleza tukio hilo kwa sasa, lakini kwa
mazingira ilivyotokea inatia mashaka makubwa na kweli tuwashukuru
vijana wa CBE ambao waliyatoa maisha yao na kuamua kumsaidia vinginevyo
wale walikuwa na nia mbaya,”alisema Mbatia.
Hata hivyo, alisema kuwa hali aliyokuwa nayo jana
Machali ilikuwa afadhali ukilinganisha na alivyokuwa juzi wakati
anapelekwa hospitalini, ambapo alimkuta akiwa amelowa damu mwili mzima
kiasi kwamba ilikuwa ni vigumu hata kumtambua.
Alipotakiwa kueleza kama tukio hilo linaweza kuwa
na uhusiano na masuala ya kisiasa, alisema ni mapema kulizungumzia jambo
hilo lakini akataka polisi waachiwe kwanza wafanye kazi yao kwani tangu
juzi walitoa ushirikiano mkubwa.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk
Nassoro Mzee, aliwaambia waandishi wa habari kuwa walimpokea Machali
juzi majira ya saa 5:00 usiku na kuwa hadi jana alikuwa akiendelea
vizuri.
Wabunge na viongozi wa Serikali jana walikuwa
wakimiminika Hospitali ya Dodoma kumjulia hali, ambapo kwa jana asubuhi
alikuwepo Mbunge Albart Ntabalima (Manyovu-CCM), Mbunge wa Kasulu
Vijijini Zaituni Buyogela (NCCR- Mageuzi) ambaye tangu juzi usiku
walikuwa wameambatana na Mbatia hadi polisi na hospitali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo ambapo hadi jana alisema tayari Polisi ilikuwa
inawashikiliwa watu wawili wakihusishwa na tukio hilo.
Kamanda Misime aliwataja watu hao ambao alisema ni
vibaka kuwa ni Jeremia Mkude (18) na Charles Chikumbili (22) ambapo
walikamatwa na misokoto ya bangi na polisi inaendelea kuwasaka
watuhumiwa wengine wawili.
Miongoni mwa waliokamatwa, mmoja Mkude alikamatwa
akiwa na jeraha usoni ambalo lilitokana na kipigo kutoka kwa watu
waliokuwa wakimsaidia Machali.
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi Mkoa Dodoma
linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kumvamia na kumshambulia Mbunge
Machali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime
alisema tukio hilo saa 1:00 jioni katika eneo la Area ‘E’ katika
Manispaa ya Dodoma wakati akirejea nyumbani kwake.
“Alikutana na vijana wanne waliokuwa wamesimama
katikati ya barabara akapiga honi lakini hawakupisha. Aliamua kuwauliza
“Jamani mnasimama katikati ya barabara si nitawagonga?” Nao wakamjibu:
“Wewe si unajifanya mtoto wa Mbunge, tutakupiga sasa”. Alisisitiza
Kamanda Misime.
Kamanda Misime alisema mheshimiwa alipojaribu kupita vijana hao walipiga gari lake.
kitu ambacho kilimfanya ashuke ili atazame kama
gari hilo limepata uharibifu wowote, ndipo vijana hao wakaanza
kumshambulia kwa ngumi na mateke huku naye akijitahidi kujihami.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, David Misime
alisema askari walipowafanyia upekuzi watuhumiwa usiku huo wa manane
walikutwa na misokoto miwili ya bangi.
1 comment:
Hakika si kitendo kizuri kwa kuwajeruhi wabunge wetu..... pole sana Mchali.....
Post a Comment