Hamed Bakayoko, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ivory Coast ametoa pendekezo
jipya la kufanyiwa marekebisho muundo wa Tume Huru ya Uchaguzi ya nchi
hiyo. Kwa mujibu wa muundo wa awali, idadi ya wajumbe wa tume hiyo
ilikuwa 31 na inapasa kupunguzwa ambapo idadi ya wawakilishi wa chama
tawala ilikuwa mara mbili ya wawakilishi ya vyama vya upinzani. Kwa
upande wa serikali, licha ya kuwepo wawakilishi watatu kutoka chama
tawala, kulikuwa na wawakilishi wengine wanne ambapo mmoja anateuliwa na
Rais, na wengine waliosalia wanatoka Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara
ya Uchumi na mwingine kutoka baraza kuu la sheria la nchi hiyo.
Hii ni
katika hali ambayo, mrengo wa upinzani na ule wa jumuiya za kiraia
zilitengewa nafasi tatu kila moja. Kwa muda mrefu sasa mrengo wa
upinzani umekuwa ukilalamikia muundo huo ambao umekuwa ukikipatia nguvu
zaidi chama tawala. Suala la kuvunjwa tume huru ya uchaguzi nchini Ivory
Coast ambayo ilitekeleza jukumu la kuendesha uchaguzi wa rais wa 2010,
uchaguzi wa bunge wa 2011 na uchaguzi wa mabaraza ya miji na serikali
za mitaa wa 2013, ni miongoni mwa matakwa yaliyotolewa na wapinzani
nchini humo. Hii ni katika hali ambayo, Chama cha Demokrasia, ambacho
kinamuunga mkono Rais Alassane Ouattara kimewatuhumu wapinzani kwamba
wanang'ang'ania mambo yasiyo na msingi wowote. Inaonekana kuwa, serikali
ya Ivory Coast imeamua kulegeza misimamo yake ya awali na kuliangalia
upya pendekezo la kufanyiwa marekebisho tume hiyo. Kwa mujibu wa
pendekezo jipya lililotolewa na Waziri Hamed Bakayoko, Tume ya Taifa ya
Uchaguzi itakuwa na jumla ya wajumbe 17, ambapo itakuwa na mwenyekiti,
wajumbe wanne kutoka serikalini, wajumbe wanne kutoka chama tawala,
wanne kutoka jumuiya za kiraia na wengine wanne watatoka kambi ya
upinzani. Pendekezo hilo la serikali la kuifanyia marekebisho tume ya
uchaguzi, litawasilishwa bungeni tarehe 19 mwezi huu. Muundo wa tume ya
uchaguzi ulikuwa mwiba na mzozo mkubwa kati ya kambi ya wapinzani na
serikali ya Ivory Coast. Weledi wa mambo wanasema kuwa, muundo mzuri na
usioegemea upande wowote, utazuia kukaririwa machafuko kama yale
yaliyotokea mwaka 2010 baada ya kufanyika uchaguzi wa rais. Licha ya
weledi hao wa masuala ya kisiasa, Umoja wa Mataifa uliwahi kusisitiza
juu ya kufanyiwa marekebisho muundo wa tume ya uchaguzi ili kuepusha
kujitokeza tena machafuko nchini Ivory Coast. Baadhi ya weledi hao
wanasema kuwa, muundo uliopita wa tume ya uchaguzi ulitoa mwanya kwa
tume hiyo kudhibitiwa na chama tawala ikilinganishwa na pendekezo jipya
la serikali. Imeelezwa kuwa, uchaguzi wa rais umepangwa kufanyika mwezi
Oktoba mwakani. Weledi wa mambo wanasema kuwa, kipindi kilichosalia hadi
kufanyika uchaguzi huo ni muhimu mno kwa wanasiasa na wananchi wa Ivory
Coast, na hasa ikizingatiwa kwamba migogoro mingi ilijitokeza nchini
humo wakati wa kipindi cha uchaguzi. Wachambuzi wa mambo wanaamini
kwamba, marekebisho ya muundo wa tume ya uchaguzi pekee hayataweza kuwa
na taathira kubwa ya kuzuia kukaririwa tena mapigano yaliyotokea miaka
iliyopita ambayo yalisababisha mamia ya maelfu ya watu kuuawa na kuwa
wakimbizi. Wachambuzi wengine wanasema kuwa, kutolewa mafunzo ya uraia
na misingi ya demokrasia na hasa mashuleni na hali kadhalika kukomeshwa
uingiliaji wa madola ya kigeni nchini Ivory Coast, ni miongoni mwa
mambo yanayoweza kudhamini amani na utulivu nchini humo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment