Waziri Mkuu wa Mali ameeleza kuwa serikali yake imejiandaa kufanya
mazungumzo na makundi ya wapinzani wenaobeba silaha huko kaskazini mwa
nchi. Moussa Mara sambamba na kukaribia kuanza kwa mazungumzo hayo,
ameelezea pia matarajio yake ya kuhitimishwa mapigano huko mjini Kidal.
Makubaliano ya usitishaji mapigano yalifikiwa wiki iliyopita huko mjini
Kidal kati ya mwakilishi wa serikali ya Bamako na makundi matatu ya
wapinzani chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika AU, hata hivyo hadi sasa
bado hayajatekelezwa.
Katika kikao cha wanachama wa Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa kilichoitishwa kwa lengo la kujadili hali ya mambo
nchini Mali, washiriki walizitaka pande mbili kutekeleza haraka
makubaliano hayo ya usitishwaji mapigano. Katika sehemu ya makubaliano
hayo ambayo yalijumuisha vipengee vinavyohusu ubadilishanaji mateka na
kuwasilisha misaada ya kibinaadamu kwa wakimbizi, kulisisitiziwa pia
kuanza mazungumzo ya pande mbili. Ni kwa ajili hiyo ndio maana weledi wa
mambo wakawa na matumaini ya kuwepo uwezekano wa kukaa pamoja pande
husika hasa kwa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya mwakilishi
wa serikali na makundi matatu ya upinzani ambayo ni Harakati ya Ukombozi
wa Azawad, Baraza Kuu la Umoja wa Azawad na Harakati ya Kiarabu ya
Wazawa wa Azawad. Pamoja na yote hayo, kuwepo tofauti kati ya makundi
hayo matatu yenye mafungamano na kabila la Tuareg linalopigania
kujitenga eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, kunaweza kupelekea
kuahirishwa mazungumzo hayo tarajiwa ya amani. Makubaliano ya mjini
Ouagadougou, Burkina Faso yaliyofikiwa mwezi Juni mwaka jana chini ya
upatanishi wa nchi hiyo, yalisisitizia pia juu ya udharura wa kufanyika
mazungumzo kuhusiana na mgogoro wa nchi hiyo. Kwa mtazamo wa weledi wa
mambo, mashirikiano ya nchi za eneo la Sahel la Afrika na halikadhalika
juhudi za nchi za magharibi mwa bara hilo katika kuharakisha mwenendo wa
amani na mazungumzo ya kitaifa kuhusiana na mgogoro wa kaskazini mwa
taifa hilo, yanatajwa kuwa yenye taathira kubwa katika kadhia hiyo.
Mbali na hayo mwaka jana katika kikao cha wakuu wa nchi za Jumuiya ya
Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS kilichofanyika mjini
Yamoussoukro, Côte d'Ivoire, sanjari na kukaribisha makubaliano ya
amani, wakuu hao walitaka kutekelezwa makubaliano hayo ya amani. Kabla
ya hapo pia viongozi wa nchi za eneo la Sahel la Afrika hapo mwezi
Januari mwaka jana walisisitizia juu ya udharura wa kudhaminiwa usalama
wa eneo hilo. Ni wazi kwamba ushirikiano wa askari wa kulinda amani wa
kimataifa kwa kushirikiana na jeshi la Mali katika juhudi za
kuyanyang’anya silaha makundi ya upinzani, kurejea katika hali ya
kawaida maisha ya wananchi, kulindwa umoja wa kitaifa na umoja wa jeshi
la nchi hiyo, ni mambo yenye umuhimu mkubwa katika kusaidia kumaliza
hali ya mchafukoge nchini humo. Hatua ya Waziri Mkuu wa Mali Moussa Mara
ya kutangaza utayarifu wa serikali yake kwa ajili ya kuanza mazungumzo
na makundi ya wapinzani wa serikali ya Bamako, inakuja kufuatia uungaji
mkono wa kisiasa wa nchi jirani na taifa hilo hasa Côte d’Ivoire na
Burkina Faso. Aidha utayarifu huo na sisitizo la serikali ya Moussa
Mara, kwa ajili ya mazungumzo hayo, limezingatia ukweli huu kwamba hivi
sasa viongozi wa nchi za eneo la magharibi mwa Afrika, wamefikia natija
hii kwamba, mgogoro wa kaskazini mwa Mali unaweza kutatuliwa tu kwa njia
za kidiplomasia. Hivyo katika kikao cha kujadili hali ya usalama wa
nchi hiyo kitakachofanyika wiki ijayo mjini Bamako, viongozi wa serikali
pia watajadili makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni na wapinzani. Na
ikiwa wapinzani watatoa jibu chanya kuhusiana na pendekezo la Waziri
Mkuu wa nchi hiyo, basi mazungumzo ya amani yatafanyika katika anga
chanya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment