Waasi wa kundi la FDLR nchini Rwanda walioko mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo wamekubali mpango wa kupokonywa silaha kwa sharti
wafanye mazungumzo na serikali ya Kigali. Taarifa zinasema kuwa, waasi
hao wameeleza kwamba, suala la kupokonywa silaha ni mwanzo wa harakati
za kurejeshwa amani na utulivu katika eneo la Maziwa Makuu ya Afrika.
Hata hivyo, waasi hao FDLR wamesisitiza kwamba, mpango huo unaweza
kufanikiwa iwapo viongozi wa serikali ya Rwanda nao watakubali kufanya
mazungumzo ya amani na waasi hao wa Kihutu.
Hivi karibuni, waasi hao
waliamua kuweka chini silaha zao na badala yake wakatangaza azma yao ya
kutumbukia kwenye uwanja wa kisiasa nchini Rwanda. Hayo yanaelezwa
katika hali ambayo, siku chache zilizopita wanamgambo wapatao 100 kundi
hilo waliweka silaha zao chini kwenye sherehe zilizofanyika katika jimbo
la Kivu Kaskazini. Jenerali Victor Byiringiro Kamanda wa wanamgambo wa
FDLR amesema kuwa, hatua hiyo imechukuliwa kwa shabaha ya kuonyesha nia
njema waliyokuwa nayo, na kuiomba jamii ya kimataifa kutekeleza majukumu
yao ya kuandaa mazingira ya kufanyika mazungumzo ya amani kati ya pande
hizo mbili. Imeelezwa kuwa sherehe hiyo ilihudhuriwa na baadhi ya
makamanda wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo
MONUSCO.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment