Mwakilishi wa kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa amelaumu msimamo
wa Baraza la Usalama la umoja huo kuhusiana na magaidi wanaofanya mauaji
nchini mwake. Bashar al Jaafari amesema, baadhi ya nchi wanachama wa
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanayaunga mkono kwa uwazi na kwa
siri makundi ya kigaidi na ndiyo maana makundi hayo yanaendelea kufanya
jinai huko Syria. Amesema, nchi hizo zinaunga mkono vitendo vya kigaidi
nchini Syria kwa kutumia nadharia ya kwamba "lengo linahalalisha njia."
Amesema nchi hizo zimeamua kutumia njia yoyote ile kufikia malengo yao
ya kisiasa hata kama njia hizo zitapelekea kuuawa maelfu ya wananchi wa
Syria.
Mwakilishi wa kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa ametoa
mfano akisema, kukatiwa maji zaidi ya wakazi milioni tatu wa mji wa
Halab na kuvurumishwa makombora kwenye mashule, Vyuo Vikuu na mikutano
ya uchaguzi ya wananchi katika mkoa wa Dar'a ni matokeo ya uungaji mkono
wa baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa
magenge ya kigaidi huko Syria. Matamshi hayo ya Bashar al Jaafari
yamekuja katika hali ambayo Umoja wa Ulaya umeamua kuongeza vikwazo
vyake dhidi ya Syria hadi mwezi Juni 2015 kutokana na serikali ya nchi
hiyo kuamua kuwapa haki yao ya kidemokrasia wananchi wa nchi hiyo ya
kuchagua kiongozi wanayemtaka. Baadhi ya duru zimesema kuwa, hatua hiyo
ya kindumilakuwili ya Umoja wa Ulaya imechukuliwa ili kukwamisha
kufanyika uchaguzi huko Syria. Ni jambo lisilo na shaka kwamba mgogoro
wa hivi sasa wa Syria unatokana na siasa za kupenda vita za baadhi ya
nchi za Magharibi pamoja na Marekani. Baadhi ya nchi za eneo la
Mashariki ya Kati na jirani na Syria nazo zinashutumiwa kushirikiana na
Marekani katika jinai zinazofanywa dhidi ya wananchi na maafisa wa
serikali nchini Syria. Mtandao wa Intaneti wa Horriyat wa nchini Uturuki
umeripoti kuwa, katika mkakati mpya wa Rais Barack Obama wa Marekani,
makundi ya kigaidi yatakuwa yanapewa mafunzo ya kijeshi nchini Uturuki.
Mtandao huo umemnukuu Ahmad Davoudoglu, Waziri wa Mambo ya Nje wa
Uturuki akisema kuwa, kuna matukio muhimu sana yatashuhudiwa karibuni
hivi nchini Syria. Matamshi hayo yakipimwa na sisitizo la Obama la
kusema kuwa atashirikiana zaidi na Uturuki kuhusu kadhia ya Syria na
wakati huo huo Rais huyo wa Marekani akatangaza kuongeza misaada yake
kwa waasi wa Syria, yanafafanua makusudio ya Waziri wa Mambo ya Nje wa
Uturuki kuhusu matukio muhimu yatakayotokea karibuni hivi nchini Syria.
Duru za habari zimefichua pia kuwa, hadi hivi sasa Marekani imeshatumia
dola milioni laki tatu kuyasaidia magenge ya kigaidi yanayofanya mauaji
nchini Syria. Nchi za Saudi Arabia, Qatar, Imarati pamoja na Uturuki
zinatajwa kuwa ni miongoni mwa nchi ambazo zinayasaidia sana magenge ya
kigaidi nchini Syria lengo likiwa ni kutaka kuvuruga uchaguzi wa rais
huko Syria. Hata hivyo, wananchi wa Syria walioko nje ya nchi hiyo
wamejitokeza kwa wingi sana katika uchaguzi huo jambo ambalo
linahesabiwa kuwa ni jibu la wazi la upinzani wa wananchi hao kwa
magenge ya kigaidi na mabwana zao na uungaji mkono wao mkubwa kwa
jitihada za serikali yao ya Syria za kupambana na magenge ya kigaidi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment