Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Monday, December 16, 2013

Ukandamizaji dhidi ya wanawake katika ulimwengu wa leo

Siku ya Jumatatu ya Novemba 25 mwaka huu, ilisadifiana na siku ya kimataifa ya kupambana na ukandamizaji dhidi ya wanawake duniani. Sherehe hizo zilifanyika sambamba na kuwakumbuka wasichana watatu raia wa nchi ya Jamhuri ya Dominica maarufu kwa jina la akina dada wa “Mirabal” waliouawa na vibaraka wa utawala wa kidikteta wa nchi hiyo mnamo tarehe 25 Novemba mwaka 1960, baada ya kupigwa vibaya, kudhalilishwa na kutukanwa. Tuhuma zilizokuwa zikiwakabili wanawake hao watatu ni kushiriki katika harakati za kisiasa dhidi ya utawala wa wakati huo nchini humo.
Ni kufuatia tukio hilo na baada ya ombi la mashirika kadhaa na wanaharakati wa kutetea haki za binaadamu duniani, ndipo mwaka 1999 Umoja wa Mataifa ukaitangaza rasmi tarehe 25 Novemba kuwa siku ya kimataifa ya kupambana na ukandamizaji dhidi ya wanawake duniani. Tangu mwaka huo siku hiyo imekuwa ikiadhimishwa kimataifa na nchi kadhaa za dunia kuwasilisha mipango mbalimbali ya kupambana na ukandamizaji huo.
Neno ‘ukandamizaji dhidi ya wanawake’ ni istilahi maalumu ambayo hutumika katika kuelezea vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeuarifisha unyanyasaji unaofanywa dhidi ya wanawake kuwa ni, “kila kitendo cha unyanyasaji wa kijinsia ambacho kinaweza kusababisha madhara ya kimwili, kijinsia au kisaikolojia kwa wanawake.” Hata hivyo suala la kusikitisha ni kwamba, hadi sasa hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa katika ulimwengu wa leo katika kuzuia vitendo hivyo, licha ya baadhi ya nchi za dunia kujinadi kupambana na ukandamiza huo dhidi ya wanawake. Suala hilo limepelekea hata baadhi ya viongozi wa Umoja wa Mataifa akiwemo Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa umoja huo, kukosoa kile kilichotajwa kuwa ni tofauti iliyopo kati ya maneno na utendaji katika kupambana na ukandamizaji dhidi ya wanawake na wasichana duniani.

Hadi sasa tukiwa katika milenia ya tatu vitendo vya ukandamizaji dhidi ya wanawake vimezidi kushika kasi. Katika maeneo kadhaa ulimwenguni, vitendo hivyo hutendeka kwa njia tofauti ukiwemo, unyanyasaji na utumwa wa ngono, unyanyasaji wa maneno, unyanyasaji unaotokana na vita, unyanyasaji wa kimpangilio, unyanyasaji wa miamala mibovu na unyanyasaji wa kisiasa. Hii leo unyanyasaji dhidi ya wanawake umekithiri sana katika nchi za Magharibi hususan Marekani. Hii ni katika hali ambayo serikali ya nchi hiyo imekuwa ikizituhumu serikali za nchi nyingine zinazopinga siasa zake kuwa zinawakandamiza wanawake. Hata hivyo taasisi za wananchi wa Marekani zinaripoti kuwa, vitendo hivyo vimeongezeka kwa kiasi kikubwa nchini humo. Moja ya vitendo vibaya vya ukandamizaji huo ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia na ufisadi wa kiakhlaqi vilivyotawala nchini Marekani. Kituo cha kukabiliana na migogoro ya unyanyasaji cha Santa Barbara nchini Marekani kimeandika ripoti kama ninavyonukuu: “Katika kila dakika 1.3 mwanamke mmoja wa Kimarekeni hukumbwa na unyanyasaji wa kijinsia na vitendo vyote hivyo hutelekezwa kikatili.” Mwisho wa kunukuu. Nayo taasisi ya Marekeni ya ‘RAINN’ ambayo inajihusisha na uchunguzi wa vitendo vya unyanyasaji, mateso na uhusiano haramu kati ya familia na jamaa, imethibitisha ripoti hiyo na kuongeza kuwa watendaji wa jinai hizo za kijinsia hawatiwi mbaroni wala kufungwa jela. Ukweli ni kwamba, kutokana na serikali ya Marekani kushindwa kuwachukulia hatua kali wahusika wa vitendo hivyo, jambo hilo limewapa ujasiri wahalifu kuendelea na jinai zao hizo.
Umoja wa Ulaya pia licha ya kupiga hatua kubwa za maendeleo ya kimaada, umeshindwa kabisa kuwalinda wanawake kutokana na ujangili huo wa kijinsia. Idadi kubwa ya wanawake wanaokumbwa na unyanyasaji wa kijinsia, kimwili na kisaikolojia katika familia za Ulaya imekuwa ni ya kutia wasiwasi. Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja huo, licha ya kuwekwa sheria kali za kuzuia unyanyasaji wa kifamilia dhidi ya wanawake barani humo, lakini vitendo hivyo vimezidi kuongezeka katika ngazi zote siku hadi siku. Kwa mfano nchini Uingereza tu, karibu kila dakika moja mwanamke mmoja huipigia simu polisi akiripoti kutendewa ukandamizaji katika familia yake. Aidha wanawake wa nchi nyingine za Ulaya nao hawajanusurika na ukandamizaji huo wa kifamilia dhidi yao. Baadhi ya nchi kama vile Sweden, Ujerumani, Ufaransa, Uhispania, Ubelgiji, Ureno, Uholanzi, Uguriki na Serbia, kunaripotiwa ongezeko kubwa la vitendo vya ukandamizaji wa kimwili na miamala mibaya dhidi ya wanawake. Kwa mfano tu nchini Italia kunaripotiwa kwamba, katika kila siku tatu mwanamke mmoja huuawa huku nchini Serbia kukisemekana kwamba asilimia 82 ya vitendo vya unyanyasaji wa kimwili dhidi ya wanawake hufanyika majumbani ambapo vingi hutekelezwa kwa kutumia silaha kama vile bastola na visu.
Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti karibu nusu ya wanawake wote walio ndani ya ndoa huko nchini India nao pia wanakabiliwa na vitendi hivyo vya unyanyasaji wa kimwili. Tafiti nyingine zinaonyesha kwamba,  asilimia 30 ya wanawake hao hukabiliwa na mahusiano ya kijinsia ya kulazimishwa. Kwa mujibu wa  ripoti ya Shirika la Afya Duniani WHO ambalo pia linapambana na vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kifamilia duniani, inaelezwa kuwa, ukatili wa mume dhidi ya mke na unyanyasaji wa kijinsia, ni vitendo ambavyo vimeenea sana dhidi ya wanawake duniani. Kwa mfano, ripoti iliyotolewa na shirika hilo inaonyesha kwamba, kiwango cha unyanyasaji wa kifamilia nchini Ethiopia, kimefikia asilimia 71. Wanawake wanaokumbwa na vitendo hivyo kwa muda mrefu huathiriwa na matatizo ya mfadhaiko wa moyo, lishe duni na msongo wa mawazo na matatizo mengineyo. Karibu asilimia 90 ya wahanga wa vitendo vya unyanyasaji wa kifamilia huko nchini China pia wanatajwa kuwa ni wanawake. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Shirikisho la Wanawake nchini China CWF mwanamke mmoja kati ya watatu ni muathirika wa ukatili wa kifamilia.
Magendo ya wanawake na utumwa wa kijinsia ni matatizo mengine ya unyanyasaji dhidi ya wanawake, vitendo ambavyo vimeongezeka sana katika nchi za Ulaya. Vitendo hivyo pia vimeshika kasi huko Marekani. Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa Lemondrop wa nchini Marekani, kila mwaka karibu watu elfu 20 husafirishwa kwa magendo nchini humo kwa kisingizio cha nafasi za kazi na masomo. Mbali na Marekani, vitendo vya magendo ya utumwa wa wanawake na wasichana vimeenea sana nchini Uingereza na nchi nyingi za Ulaya. Tukitoka Magharibi, nchi za Mashariki ya Kati ikiwemo Saudi Arabia, Bahrain na Misri ni nchi ambazo zimeshamiri vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake. Ni wazi kwamba, kutozingatiwa haki za msingi za binadamu na za wanawake, ni sababu ya kuongezeka vitendo hivyo katika nchi hizo. Hadi sasa wanawake wa Saudia bado wananyimwa haki zao za kimsingi kabisa. Mfalme wa nchi hiyo amepitisha sheria ambayo inawanyima wanawake haki za kimsingi kabisa ikiwemo ya kuendesha gari huku wakitakiwa kufanya kazi nyingi za nje ya nyumba kwa idhini ya waume zao. Kutokana na sheria kali za kuwazuia kuendesha magari, wanawake wa Saudia hulazimika kwenda nchi nyingine kwa ajili ya kusomea udereva na kupata leseni za kuendesha gari. Hii ni katika hali ambayo hivi karibuni Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa lilipasisha mapendekezo likiitaka nchi hiyo iboreshe hali ya haki za kibinaadamu nchini sanjari na kuitaka ikomeshe ubaguzi na ukandamizaji dhidi ya wanawake.
Ukandamizaji unaotokana na vita ni miongoni mwa matatizo mengine yanayowakabili wanawake duniani. Licha ya kwamba wanawake huwa hawana nafasi yoyote katika mizozo ya silaha, lakini wao na watoto wadogo wamekuwa wahanga wakubwa wa mizozo hiyo. Hivi sasa wanawake na mabinti wengi wa Kiislamu huko Palestina, Gaza, Lebanon, Iraq, Syria, Afghanistan na Pakistan, ni wahanga wakubwa wa ukandamizaji na ukatili unaotokana na vita. Wanawake na watoto wa Myanmar pia hawajasalimika na unyanyasaji na ukandamizaji huo. Wanawake na watoto wamekuwa wahanga wakubwa wa mauaji ya umati yanayofanyika nchini humo dhidi ya jamii ndogo ya Waislamu. Aidha huko Gaza na Palestina kwa ujumla, wanawake na wasichana wamekuwa wahanga wakubwa wa mashambulizi ya utawala katili wa Kizayuni, ambapo wengi wao wameuawa, kujeruhiwa, kufungwa jela na kufanywa wakimbizi. Wakati hayo yakijiri, kwa upande mwingine unyanyasaji wa kijinsia umeibuka katika nchi za Mashariki ya Kati kufuatia jinamizi la vitendo vya uharibifu vya Uwahabi na makundi ya kufurutu mipaka. Kwa masikitiko makubwa fatwa iliyotolewa na sheikh mmoja wa Kiwahabi wa nchini Jordan aliyehalalisha kutekwa nyara na kubakwa mabinti wa Kiislamu huko nchini Syria, imepelekea kuongezeka jinai na ukatili dhidi ya wanawake wa nchi hiyo inayoshuhudia vita vya ndani. Suala hilo limezidi kushika kasi kiasi kwamba hivi karibuni shirika moja la nchini Misri lilitangaza wazi kuwashikilia mabinti wa Syria kwa ajili ya kuwapelekea wanaume wapenda anasa na wazinifu wanaodai kupigana jihadi huko Syria. Katika ripoti yake shirika hilo lilitangaza kuwa, lina wasichana wavaa hijabu na niqab kutoka Syria kwa kiwango kinachohitajika. Huu ni ukatili wa kijinsia wa hali ya juu na wa wazi dhidi ya wanawake katika zama hizi. Inawezekana vipi katika karne hii ya 21 kutangazwa wazi wazi unyanyasaji wa kuchupa mipaka wa aina hiyo dhidi ya wanawake mbele ya kimya cha jamii ya kimataifa? Kama hiyo haitoshi, kiongozi mmoja wa Kiwahabi amewataka wanawake kwenda nchini Syria kwa ajili ya kuwaridhisha kijinsia wapiganaji wa kigaidi nchini humo. Wasichana wengi walioathiriwa na fatwa hiyo kwa siku moja walikuwa wakiingiliwa kingono na wanaume kadhaa tofauti ambapo baadhi yao walifichua jinai hizo baada ya kurejea makwao kutoka Syria.
Wapenzi wasikilizaji, kipindi chetu cha makala ya wiki kinaishia hapa kwa leo. Ni matumaini yangu kuwa mmenufaika vya kutosha na makala hii. Mimi ni Sudi Jafar Shaban, msikose kuungana nami tena katika kipindi kingine cha makala ya wiki katika siku na saa kama hii, hadi wakati mwingine ninakuageni kwa kusema, kwaherini.

No comments: