Matokeo ya duru ya pili ya uchaguzi wa Bunge nchini
Mali yanaonesha kuwa chama tawala nchini humo kimeshinda uchaguzi huo.
Chama cha Muungano kwa Ajili ya Taifa (RPM) kimejinyakulia viti vingi
zaidi vya Bunge la taifa la nchi hiyo. Ripoti zinasema kuwa, chama cha
RPM kimepata viti 60 kati ya viti 147 katika duru ya pili ya uchaguzi wa
Bunge uliofanyika siku ya Jumapili. Imeelezwa kuwa, chama cha Muungano
kwa Ajili ya Demokrasia ya Kitaifa ambacho ni muitifaki wa chama pia
kimeshinda viti 50.
Kwa msingi huo, chama tawala cha Rais wa Mali pamoja
na waitifaki wake vimepata jumla ya viti 110 vya Bunge. Chama cha URD
cha Soumaila Cisse mgombea aliyeshindwa katika uchaguzi wa rais,
kimepata viti 19 katika duru ya pili. Baraza la Katiba la Mali lenye
jukumu la kutangaza matokeo ya uchaguzi wa Bunge siku kadhaa zilizopita
lilitangaza ushindi wa wagombea 20 katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo
na kusema kuwa, kura zitapigwa tena ili kuwatafuta washindi wa viti 127
vilivyobakia.
Matokeo hayo yaliyotangazwa yatakuwa rasmi baada ya
kupasishwa na Mahakama ya Katiba. Ripoti zinaeleza kuwa uchaguzi huo wa
duru ya pili ulifanyika kwa utulivu bila matukio yoyote ya vurugu.
Mashambulizi yaliyofanywa na makundi ya wapinzani siku moja kabla ya
uchaguzi huo kwa kiasi fulani yaliwatia hofu watu na kuwazuia kwenda
vituoni kupiga kura. Mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa katika gari
kaskazini mwa Mali asubuhi siku moja kabla ya uchaguzi huo, uliharibu tu
jengo la benki katika mji wa Kidal. Kwa msingi huo idadi ya wananchi
walioshiriki katika duru ya pili ya uchaguzi wa Bunge wa Mali ilikuwa
ndogo na kiwango cha ushiriki kilikuwa cha asilimia 38.62.
Kiongozi wa timu ya wasimamizi wa Umoja wa Ulaya katika
uchaguzi wa Mali, Louis Michel amesema kuwa, uchaguzi huo kwa ujumla
ulifanyika vizuri. Michel ameeleza kuwa, uchaguzi huo ulitimiza vigezo
vya kimataifa vya uchaguzi wa kidomekrasia. Wasimamizi 3,300 na
wasimamizi wakuu 200 walihudhuria katika maeneo 54 ya uchaguzi, wakati
wa zoezi la kupiga kura nchini Mali.
No comments:
Post a Comment