Karibuni wapenzi wasikilizaji katika makala hii maalumu
tuliyokuandalieni kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na
Umaskini. Ni matumaini yetu mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi.
Tarehe 17 Oktoba ambayo mwaka huu imesadifiana na siku ya Alkhamisi,
huadhimishwa kila mwaka kwa jina la Siku ya Kimataifa ya Kupambana na
Umaskini.
Umoja wa Mataifa ndio uliotangaza siku hiyo kwa lengo la
kuzijumuisha pamoja nguvu za mataifa yote ya dunia katika jambo moja,
nalo ni kupambana na umaskini. Kila mwaka siku hiyo hutumiwa kutangaza
mshikamano wa mataifa yote ya dunia kwa ajili ya kuwaliwaza na
kuwasaidia wahanga wa ukata na majanga ya njaa na vile vile kutafuta
njia za kuweza kung'oa kikamilifu mizizi ya umaskini na ubaguzi na
kuleta heshima na utukufu wa mwanadamu.
Msingi wa kutengwa tarehe 17 Oktoba kuwa Siku ya Kimataifa ya
Kupambana na Umaskini umeanzia tangu mwaka 1987. Mwaka huo mamia ya
maelfu ya watu walikusanyika mjini Paris Ufaransa kwa ajili ya
kuadhimisha siku ya kupitishwa Hati ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa
Mataifa mwaka 1948. Watu waliokusanyika mjini Paris walipitisha kwa
kauli moja kuwa umaskini ni aina fulani ya uvunjaji wa haki za binadamu
na kwamba haiyumkiniki kulindwa haki za binadamu madhali umaskini
ungalipo duniani. Tangu mwaka huo, taasisi nyingi duniani zilianza
kuendesha kampeni ya kuwaelimisha na kuwaamsha walimwengu kuhusu
majakamoyo ya umaskini na ilipofika tarehe 17 Oktoba mwaka huo, Baraza
Kuu la Umoja wa Mataifa likaitangaza rasmi siku hiyo kuwa ni Siku ya
Kimataifa ya Kupambana na Umaskini. Suala la kupambana na umaskini
lilipata nguvu sana kuanzia mwaka 2000 wakati ilipopasishwa Hati ya
Milenia ambayo moja ya malengo yake makuu lilikuwa ni kuhakikisha
umaskini umepungua kwa kiwango kikubwa duniani ifikapo mwaka 2015. Ni
vyema kusema hapa kwamba, licha ya kuweko jitihada mbalimbali za
kufanikisha malengo ya milenia ya kukata mizizi ya umaskini duniani,
lakini hadi hivi sasa asilimia 20 ya walimwengu wanaishi kwenye umaskini
mutlaki. Umoja wa Mataifa unaendesha miradi mbalimbali ya kufanikisha
malengo ya milenia yanayotakiwa kufikiwa ifikapo mwaka 2015 ukiwa na
matumiani kwamba ifikapo mwaka huo, utakuwa umefanikiwa kupungaza
umaskini kwa kiwango kikubwa duniani. Hata hivyo kutokana na kushindwa
kufikiwa malengo hayo, hivi sasa Umoja wa Ulaya umekuja na fikra
nyingine ya kupunguza umaskini katika muongo ujao. Tab'an kuna mafanikio
ya kiasi fulani yamepatikana katika jitihada za kupambana na umaskini.
Hilo linathibitishwa na Mkuu wa Benki ya Dunia aliposema: "Sisi katika
kipindi cha miaka mitatu iliyopita, tumeshuhudia harakati za kihistoria
ambazo zimepelekea kupungua idadi ya watu wanaoishi kwenye umaskini,
lakini bado kuna watoto wadogo duniani ambao wanaishi katika ukata wa
kupindukia ambao bila ya shaka yoyote hakuna kazi iliyofanyika kwa ajili
yao." Mwisho wa kunukuu.
Bila ya shaka yoyote neno umaskini ni maarufu na kila mmoja analijua
neno hilo. Lakini ni nini maana ya watu maskini? Inaposemwa watu hawa ni
maskini kwa mujibu wa maana iliyotolewa kimataifa ni kwamba hao ni
watu, au kaya, au familia, au kundi la watu ambao vyanzo vyao vya
kiutamaduni, kimaada na kijamii ni vichache kiasi kwamba wanashindwa
kufaidika na suhula za chini kabisa katika maisha yao jambo ambalo
linawapambanua na watu wengine wanaoishi nao katika jamii. Ili kutoa
ufafanuzi zaidi, Umoja wa Mataifa umetoa maana jumla ukisema kuwa, nchi
zenye pato la wastani na la juu inabidi familia za watu wa nchi hiyo
wanaoishi kwa pato la chini ya asilimia 50 hadi asilimia 60 ya wastani
wa pato la nchi wahisabiwe kuwa ni watu maskini. Amma kwa upande wa nchi
zenye pato dogo zaidi, watu wanaoishi kwa kipato cha chini ya dola 1.25
kwa siku wanahesabiwa kuwa ni maskini. Licha ya kwamba kumefanyika
jitihada mbalimbali za kupambana na umaskini, lakini hadi hivi sasa bado
asilimia 20 ya watu duniani wanaishi kwa pato la chini ya kiwango hicho
tulichokitaja, hivyo wanahesabiwa kuwa wanaishi chini ya mstari wa
umaskini. Hii ni katika hali ambayo karibu watoto milioni 7 wa chini ya
umri wa miaka mitano wanasumbuliwa na lishe duni. Kwa mujibu wa malengo
mapya ya Benki ya Dunia, inabidi ifikapo mwaka 2030 idadi ya watu
maskini duniani ipungue kwa asilimia tatu. Jim Yong Kim, Mkuu wa Benki
ya Dunia amesema kuwa, nchi 188 duniani ambazo ni wanachama wa taasisi
hiyo ya kimataifa ya fedha zinapaswa kufanya jitihada zao zote na
kuongeza kasi katika juhudi zao za kuangamiza umaskini. Amesema, kuna
wajibu kwa nchi hizo kushirikiana vilivyo kuhakikisha kuwa malengo ya
mwaka 2030 ya benki hiyo yanafikiwa. Aidha amesema, kupambana na ukata
na kuleta ustawi kwa vizazi vijavyo ni miongoni mwa malengo makuu ya
Benki ya Dunia.
Kiujumla ni kuwa, umaskini ni miongoni mwa mambo tata sana
yanayomsumbua mwanadamu. Sababu yake ni kuwa, sababu zinazopelekea
kutokea umaskini ni nyingi sana. Hazihusiani na makosa ya kibinadamu tu,
bali umaskini unachangiwa pia na masuala ya kimaumbile kama vile ukame,
ukosefu wa mvua, maradhi katika mimea, nzige n.k. Sababu nyingine ni
wanadamu wenyewe. Madhalimu wanawanyonya wanyonge na kujilimbikizia
utajiri peke yao huku walimwengu wakiteseka kwa umaskini. Umaskini nao
si kitu cha kupita na wala si kitu cha muda mfupi, bali ni kitu ambacho
vizazi kwa vizazi vya wanadamu vinarithishana umaskini. Wataalamu
wanasema kuwa, ni vigumu kumaliza ukata na umaskini duniani ila kwa
kuwekeza kwenye watoto wadogo kwa ajili ya vizazi vijavyo. Wanasema
inabidi uweko uadilifu katika upatikanaji na utumiaji wa suhula
mbalimbali muhimu kama vile elimu bora, huduma za afya, uwekezaji,
usalama, kujenga misingi madhubuti ya kifamilia n.k. Hivyo tunathubutu
kusema kuwa, watu wanaoteseka kwa umaskini hivi sasa, wanahitajia zaidi
misaada ya kweli ya kivitendo kulikoni maneno ya kuwaliwaza tu.
Ukitoa njia tuliyotangulia kusema ya kuwekeza katika watoto wadogo,
kuna njia nyingine nyingi za kuweza kuumaliza kabisa umaskini duniani.
Kuna haja ya kufanyika jitihada za kweli za kutoka kwenye umaskini
kuelekea kwenye ustawi na maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiutamadunia
katika nchi zilizobaki nyuma kimaendeleo. Jamii yeyote ambayo uchumi
wake haukuwi, kwa kweli uwezo wake wa kujiletea maendeleo ya kiuchumi ni
mdogo na haiwezi kunyanyua kiwango cha ustawi wa watu yake. Uzoefu
unaonesha kuwa, silaha bora kabisa ya kupambana na adui umaskini ni
kuandaa fursa za kazi kupitia kuongeza uwekezaji katika sekta za viwanda
na kilimo, sambamba na kuanzisha maeneo ya uzalishaji bora na
kushirikishwa vilivyo mataifa ya dunia katika mabadilishano ya
kimataifa. Juhudi za kuleta uadilifu wa kijamii na kugawanywa kiuadilifu
utajiri kati ya matabaka mbalimbali ya watu kwenye jamii, nazo zina
umuhimu mkubwa sana katika kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa
umaskini duniani. Hata hivyo, siasa za kikoloni za nchi zinazopenda
makuu nazo zinachangia pakubwa katika kufukarika na kuwa maskini
kupindukia mataifa mengine. Ni jambo lililo wazi kuwa madola ya kibeberu
ndiyo kikwazo kikuu kinachokwamisha juhudi za kupambana na umaskini
duniani. Bila ya shaka yoyote iwapo nchi za kibeberu zitaachana na siasa
zao za kutenga fedha nyingi kugharamia masuala ya kijeshi, zitasaidia
sana katika kumaliza umaskini ulimwenguni. Ni jambo lisilo na shaka pia
kwamba, kusamehewa madeni yao nchi maskini na kuandaliwa uwanja wa
kuweza nchi hizo kufaidika na teknolojia za kisasa, nayo ni njia
nyingine inayoweza kuondoa umaskini ulimwenguni. Ni kwa sababu hii ndio
maana kichwa cha maneno cha makala yetu hii kikawa: Tunao uwezo wa
kukomesha umaskini duniani. Naam, kama kutakuwepo siasa sahihi, na iwapo
mataifa ya dunia yataheshimu makubaliano ya kimataifa na endapo
litapigwa vita kikamilifu suala la kutumiwa fedha nyingi katika masuala
ya kijeshi na kuingilia mambo ya ndani ya mataifa mengine kwa ajili ya
kuyakoloni, basi bila ya shaka yoyote jakamoyo la ukata na umaskini
linaweza kuondoka kikamilifu duniani.
No comments:
Post a Comment