Kwa mara nyingine tena jana Ijumaa, wananchi wa Beirut mji mkuu
wa Lebanon walishuhudia mripuko mkubwa wa bomu uliosababisha vifo vya
watu wasiopungua wanane akiwemo Muhammad Shatar, waziri wa zamani wa
fedha katika serikali ya Fouad Siniora na makumi ya wengine kujeruhiwa.
Lebanon ambayo kipindi fulani ilijulikana kama ardhi nyeupe katika eneo
la Mashariki ya Kati, hivi sasa inakabiliwa na hali ya ukosefu wa amani
na utulivu na inalengwa na mashambulizi ya miripuko ya mabomu yanayoua
na kujeruhi mamia ya watu wasio na hatia.
Miongoni mwa watu waliouawa
kwenye miripuko mbalimbali iliyotokea nchini humo, wako shakhsia wa
kisiasa na kijeshi, kama Hassan al Lakkis, kamanda wa ngazi za juu wa
Hizbullah ya Lebanon na Sheikh Ibrahim Ansari aliyekuwa Mkuu wa Kitengo
cha Utamaduni cha ubalozi wa Iran mjini Bairut.
Lebanon iko tofauti kabisa na nchi nyingi za Kiarabu, kwani nchi hiyo
haitawaliwi kidikteta na wala haikabiliwi na malalamiko ya mara kwa
mara ya wananchi dhidi ya serikali. Mzunguko katika muundo wa kisiasa
na kiuongozi uko wazi kabisa nchini humo. Wananchi wa Lebanon si wageni
hata kidogo katika masuala ya uchaguzi na hata ushiriki wao katika
uwanja wa kisiasa. Tunaweza kusema kuwa, Lebanon kwa miaka kadhaa sasa
inaonekana kuwa mstari wa mbele katika kupiga hatua za kisiasa na
kuimarisha muundo wa taasisi za kiraia, ikilinganishwa na nchi nyingine
za Kiarabu na hasa zile zenye ushawishi mkubwa katika eneo la Mashariki
ya Kati.
Alaa kulli haal, sababu kuu ya kukosekana amani na utulivu nchini
Lebanon inatokana na hitilafu za kisiasa na hujuma za makusudi
zinazofanywa na makundi ya kisiasa na hasa mrengo wa al Mustaqbal
kuhusiana na suala la kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa, hujuma
ambazo bila shaka zina maslahi kwa baadhi ya nchi za Kiarabu na utawala
wa Kizayuni wa Israel. Hakuna shaka kuwa, mivutano ya kisiasa na
kutoundwa serikali ya Tammam Salam Waziri Mkuu mteule, ni moja kati ya
sababu kuu za kuongeza machafuko katika maeneo mbalimbali nchini
Lebanon.
Waokoaji wakifuatilia tukio hilo. |
Suala jingine ambalo hatupaswi kulipuuza ni hili kwamba, hivi sasa
Lebanon inaathiriwa mno na machafuko yanayoendelea nchini Syria.
Serikali ya Lebanon ni miongoni mwa nchi chache ambazo tokea yalipoanza
machafuko nchini Syria, daima imekuwa mstari wa mbele kupinga uingiliaji
wa madola ya kigeni kwenye mgogoro wa nchi hiyo. Wakati mipaka ya nchi
kama Jordan na Uturuki imekuwa wazi na inatumiwa kupitisha silaha
zinazopelekwa kwa makundi ya kigaidi yanayopigana na serikali ya Rais
Bashar Assad, Lebanon haikutoa fursa hata kidogo ya kutumiwa mipaka yake
kwa lengo la kuwapelekea silaha magaidi na mamluki wa nchi za Magharibi
na za Kiarabu huko Syria. Hali kadhaika, hatua ya Hizbullah ya
kulisaidia jeshi la Syria baada ya utawala wa Israel kushambulia vituo
vya kiutafiti, iliongeza nguvu za kijeshi za Syria katika kukabiliana na
makundi ya kigaidi, jambo ambalo lilizichukiza nchi za Magharibi na
vibaraka wao wa Kiarabu na huenda suala hili ndiyo sababu ya kuongezeka
operesheni za kigaidi ndani ya ardhi ya Lebanon. Baadhi ya makundi ya
kigaidi ya Syria yaliwapeleka wanamgambo wao ndani ya ardhi ya Lebanon
ili kutekeleza operesheni za kigaidi nchini humo. Makundi mengine
yanayofungamana na mitandao ya kigaidi yanafanya juhudi za kuweka kambi
zao ndani ya ardhi ya Lebanon.
Imeelezwa kuwa, lengo la kuwepo magaidi ndani ya ardhi ya Lebanon ni
kutoa pigo kwa Hizbullah na kuzidisha operesheni za kigaidi dhidi ya
shakhsia wa kisiasa na kijeshi wa Lebanon ili jeshi la nchi hiyo
lielekeze nguvu zake zaidi ndani katika kukabiliana na makundi ya
kigaidi na kuacha kushughulikia maeneo ya mipakani, ili makundi hayo ya
kigaidi yapate mwanya wa kupitisha silaha zao na kuzipeleka Syria.
Nukta muhimu nyingine ya kuzingatiwa ni kwamba, Sirajuddin Zuraiqat
kiongozi wa kundi la kigaidi linalowakufurisha Waislamu, siku ya
Alhamisi iliyopita alitoa mkanda wa video na kutishia kwamba, Beirut
itashuhudia miripuko mipya ya kigaidi hivi karibuni.
Ni kwa kuzingatia ushahidi huo, ndipo tukamuona Adnan Mansour Waziri
wa Mambo ya Nchi za Nje wa Lebanon katika radiamali yake aliyoitoa mara
baada ya mripuko huo wa jana akasema kuwa, mripuko huo ni katika
taathira za mgogoro wa Syria. Naye Shakib Qortbawi Waziri wa Sheria wa
Lebanon amesema kuwa, mripuko huo umeongozwa kutoka nje ya nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment