Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena limeitisha
kikao na kujadili kadhia ya Syria. Kikao hicho cha faragha cha Baraza la
Usalama kilifanyika jana huku mada mbili kuu zikitawala mkutano huo.
Maudhui ya kwanza iliyojadiliwa katika mkutano huo ni silaha za kemikali
zilizotumika Syria na mkutano wa Geneva-2. Nukta muhimu katika kikao
hicho ni kwamba, mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa alizikosoa
vikali siasa na misimamo ya Marekani kuhusiana na mgogoro wa Syria.
Vitaly Ivanovich Churkin, ameituhumu Marekani kwamba, imepuuza takwa la
Russia la kuitaka Washington itoe nyaraka na ushahidi wa kuonesha
kwamba, serikali ya Syria ilitumia silaha za kemikali dhidi ya raia.
Amesema, madai ya Marekani kwamba, serikali ya Syria ilihusika na
shambulio hilo hayakinaishi na kwamba, Moscow inaamini kwamba, shambulio
hilo la kichochezi lilifanywa na wanamgambo wanaobeba silaha nchini
Syria. Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema kwamba,
Moscow ina ushahidi unaoonesha kwamba, kuanzia Disemba mwaka 2012,
serikali ya Marekani ilikuwa na taarifa kuwa, muda si mrefu mashambulizi
ya silaha za kemikali yatafanyika nchini Syria. Swali la kimsingi ni
kwamba, kwa nini Washington ilinyamaza kimya licha ya kuwa na taarifa
kuhusiana na jambo hilo? Baadhi ya duru zinapinga madai ya Marekani
kwamba, serikali ya Syria ndiyo iliyohusika na shambulio la silaha za
kemikali za gesi ya Sarin.
Kuuawa wanajeshi wa serikali na raia katika
mashambulio tofauti ya kemikali nchini Syria na ushirikiano mkubwa
uliooneshwa na serikali ya Rais Bashar al-Assad kwa wakaguzi wa Umoja wa
Mataifa sambamba na kukubaliana serikali hiyo na suala la kuangamizwa
silaha hizo ni ushahidi tosha kwamba, serikali ya Damascus haikuhusika
na shambulio hilo. Katika upande wa pili, kwa kuzingatia kwamba, daima
wanamgambo wanaobeba silaha nchini Syria wamekuwa wakitafuta kisingizio
ili Syria ivamiwe kijeshi na madola ya kigeni, dhana ya kwamba, waasi
hao ndio waliohusika na shambulio la kemikali inazidi kupata nguvu. Hasa
kwa kutilia maanani kwamba, ushahidi unaonesha kuwa, hakuna jinai
nchini Syria ambayo haijafanywa na magaidi na waasi hao. Duru za kitiba
nchini Syria zimetangaza kwamba, raia 80 wameuawa kwa umati na magaidi
hao katika eneo la Rif Dimashq. Je makundi ya kitakfiri yanaofanya jinai
kama hizo hayawezi kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia na askari
wa serikali? Nukta ya kutaamali zaidi ni kwamba, jinai kama hizo
zimekuwa zikifanyika kwa baraka na idhini ya Marekani. Serikali ya
Marekani ni miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa magaidi wa Syria katika
kipindi cha miaka hii mitatu ya mgogoro huo. Hivi sasa pia ambapo kuna
juhudi za kuhakikisha kunafanyika mkutano wa Geneva-2 kwa shabaha ya
kuupatia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa Syria, Marekani ndio kwanza
wanaendelea kuzungumzia udharura wa kuungwa mkono makundi ya kigaidi
nchini Syria.
No comments:
Post a Comment