Utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain unafuta alama za Kiislamu kwa
kujenga majengo na bustani za kupumzikia mahala ulipobomoa misikiti
katika harakati za mapinduzi ya wananchi nchini humo. Mtandao wa mrengo
wa upinzani wa Februari 14, umewanukuu wakazi wa kijiji cha Aali
wakisema kuwa, utawala wa Aal Khalifa unajenga jengo katika eneo
kulipobomolewa na askari wa utawala huo, msikiti wa Amir al-Barghuthi.
Hii ni katika hali ambayo licha ya kubomolewa msikiti huo, wakazi wa
kijiji hicho bado wanasali katika eneo hilo. Viongozi na shakhsia wa
kidini nchini Bahrain wamesisitiza kwa mara kadhaa kuwa, hakuna mtu
mwenye haki ya kuhodhi na kutumia hata dhiraa ya ardhi ya kidini hata
kama ni mahala ilipobomolewa misikiti na askari wa utawala wa kidikteta
wa nchi hiyo. Mashirika mbalimbali ya Kimataifa na lile la Umoja wa
Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa pamoja yamelalamikia
hatua ya utawala wa Aal Khalifa ya kubomoa misikiti ya kale nchini
humo. Kabla ya hapo Baraza la Kiislamu na kituo cha watetezi wa haki za
binaadamu nchini humo yalikuwa yametangaza kuwa, mkuu wa kongresi ya
kijamii ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni
(UNESCO) anazo taarifa kuhusiana na jinai za utawala wa Aal Khalifa za
kubomoa msikiti wa kihistoria wa al-Berighi uliojengwa mnamo mwaka 1549
yaani miaka 464 iliyopita. Katika ripoti iliyowasilishwa kwenye ofisi ya
UNESCO, Sheikh Maitham al-Selman kiongozi wa kitengo kinachohusika na
uhuru wa kuabudu katika kituo cha watetezi wa haki za binaadamu nchini
Bahrain ameeleza kuwa jumla ya misikiti 38 imebomolewa na utawala wa
nchi hiyo.
Kabla ya hapo pia na licha ya kuwepo upinzani mkubwa wa
wananchi, utawala huo ulikuwa umeanza shughuli za ujenzi wa bustani ya
kupumzikia katika eneo la msikiti wa Abudharri. Msikiti huo ulibomolewa
na askari watiifu kwa utawala wa kifalme wa Aal Khalifa miaka miwili
iliyopita baada ya kutangazwa kwa hali ya hatari nchini Bahrain.
Kuhusiana na hali hiyo Jumuiya ya Kitaifa ya al Wifaq imetoa ripoti ya
kulaani ubomoaji misikiti nchini humo na kusema, mashambulizi dhidi ya
Husseiniya na kubomolewa majengo hayo ya kidini ni miongoni mwa jinai za
utawala wa Aal Khalifa ambazo zimekuwa zikitekelezwa kwa kipindi cha
miaka mitatu ya hivi karibuni dhidi ya matukufu ya kidini. Sheikh Ali
Salman amesema kuwa, katika kipindi cha vuguvugu la mapinduzi ya Bahrain
wananchi hawajawahi kufanya shambulizi lolote dhidi ya msikiti. Hii ni
katika hali ambayo utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa umeshabomoa
makumi ya misikiti na Husseiniya ikiwemo pia misitiki ya kihistoria.
Kwa upande mwingine Sheikh Maitham al-Selman ambaye pia ni mjumbe wa
kituo cha haki za binaadamu nchini Bahrain, ametaka kuundwe tume huru ya
kimataifa ya uchunguzi ili kukomesha mara moja mashambulizi dhidi ya
maeneo ya ibada katika maeneo tofauti ya Bahrain. Aidha kiongozi huyo
ametaka kukomeshwa uchochezi wa kikaumu na kimadhehebu unaofanywa
kupitia vyombo vya habari mbalimbali nchini Bahrain. Tangu mwaka 2011
lilipoanza vuguvugu la mapinduzi ya wananchi wa Bahrain utawala wa
kidikteta wa Aal Khalifa umebomoa makumi ya misikiti ya Waislamu wa
Kishia katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na kukataa kuijenga tena
misikiti hiyo katika maeneo hayo.
No comments:
Post a Comment