Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Saturday, December 7, 2013

UN: Uchunguzi ufanyike kuhusu kuuzwa Warohingya

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusiana na kuweko ripoti kwamba, idara ya uhamiaji ya Thailand imekuwa ikishirikiana na magenge ya magendo ya binadamu kuwauza wakimbizi kutoka Myanmar ambao ni Waislamu wa kabila la Rohingya. Umoja wa Mataifa umesisitiza kwamba, umesikitishwa na ripoti hiyo inayoeleza kwamba, maafisa wa idara ya uhamiaji ya Thailand wamekuwa wakiwauza kwa magenge ya magendo ya binadamu Waislamu wa kabila ya Rohingya wanaoomba hifadhi katika nchi hiyo.
Vivian Tan, Msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amesema kuwa, kuna haja ya kufanyika uchunguzi kuhusiana na madai hayo. Amesema, daima Umoja wa Mataifa umekuwa ukizitaka nchi za jirani na Myanmar kuwapatia hifadhi ya muda Waislamu wa Rohingya na kuwalinda pia na kwamba, kuwalinda huko kunajumuisha pia suala la kuwakinga na utumiaji mbaya wa aina yoyote. Tangu mwezi Juni mwaka jana magaidi wa Kibudha wamekuwa wakiwashambulia Waislamu wa kabila la Rohingya katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar ambapo hadi sasa maelfu ya Waislamu wameuawa huku wengine karibu laki mbili wakiachwa bila makao. Waislamu hao wamekuwa wakilazimika kukimbilia katika nchi za Thailand na Malaysia.

No comments: