Jenerali David Sejusa, mkuu wa zamani wa vyombo vya kiintelijensia
nchini Uganda ametangaza kuwa, ameanzisha chama kipya cha kisiasa cha
upinzani. Jenerali huyo mstaafu aliyekimbilia nchini Uingereza,
amewaambia waandishi wa habari mjini London kwamba, anapanga kugombea
kiti cha Urais katika uchaguzi ujao kwa tiketi ya chama chake cha The
Freedom and Unity Front. Weledi wa mambo wanaamini kwamba, kuundwa
chama kipya cha kisiasa nchini Uganda hakuna maana si jaribio la
kumuondoa Rais Museveni katika ulingo wa kisiasa, bali ni hatua moja
mbele ya kutaka kumuweka kando mtoto wa Rais Museveni ambaye anataka
kuwania kiti cha Urais nchini Uganda katika uchaguzi ujao uliopangwa
kufanyika mwaka 2016.
Hii ni katika hali ambayo, mwana wa Rais Museveni,
Brigedia Muhoozi Kainerugaba hadi sasa hajakanusha tetesi za kutaka
kugombea kiti cha Urais katika uchaguzi ujao nchini Uganda. Weledi wa
mambo ya kisiasa wanaamini kuwa, kupandishwa vyeo haraka haraka jeshini
mwana huyo wa Museveni kunaashiria kuwa anaandaliwa kumrithi baba yake.
Hasa kwa kutilia maanani kwamba, washauri wa Rais Museveni hawaoni kama
Museveni ana hamu ya kugombea tena Urais kwa mara ya tano mfululizo.
Wapinzani nchini Uganda wanalalamika kuwa, kipindi cha karibu miaka 28
cha utawala wa Rais Museveni kimeambatana na kukandamizwa vibaya
wapinzani pamoja na wakosoaji wa serikali yake. Wapinzani hao wanatoa
mfano wa kufutwa kazi Erias Lukwago, aliyekuwa meya wa Kampala wakisema
kuwa huo ni ushahidi tosha wa kuthibitisha madai yao hayo. Daktari Kizza
Besigye kiongozi wa zamani wa FDC na mpinzani mkuu wa Museveni
ameshindwa mara tatu katika kinyang'anyiro cha Urais.
Katika uchaguzi
uliopita uliofanyika mwaka 2011, Rais Museveni alipata asilimia 68 ya
kura na kumshinda kwa mara nyingine tena hasimu wake wa kisiasa Kizza
Besigye aliyepata asilimia 26 ya kura. Pamoja na hayo waangalizi wa
uchaguzi huo kutoka Umoja wa Ulaya walitangaza kuwa, hatua ya serikali
ya Uganda ya kusambaza askari katika barabara za Kampala na katika miji
mikubwa ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki ililenga kuzusha woga na wasi
wasi baina ya wananchi katika siku ya kupiga kura. Wakosoaji wa serikali
ya Uganda wanaamini kwamba, kukandamizwa wapinzani na wanaharakati wa
kisiasa wa Uganda ndio udhaifu mkubwa wa serikali ya Rais Museveni.
Baada ya Rais Museveni kuingia madarakani mwaka 1986, alipiga marufuku
shughuli za vyama vya kisiasa. Hata hivyo mashinikizo ya kieneo na
kimataifa yalimuelemea na ndio maana mwaka 2005 alilazimika kufungua
mlango vyama vya kisiasa na kuviruhusu kuendesha shughuli zao. Hivi sasa
kuna vyama vingi vya kisiasa nchini Uganda lakini havina nguvu za
kushindana na chama tawala cha NRM katika uchaguzi. Baadhi ya wachambuzi
wa mambo wanasema kuwa, kuanzishwa chama kipya cha kisiasa na Jenerali
David Sejusa mkuu wa zamani wa vyombo vya kiintelejensia nchini Uganda
kunaweza kutathminiwa kuwa ni changamoto nyingine kubwa kwa chama tawala
katika uchaguzi ujao.
No comments:
Post a Comment