Huku mwaka wa 2013 ukiwa umefikia katika siku zake za mwisho, Ofisi ya
Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa, mwaka 2013
utawala wa Kizayuni wa Israel umewafanyia ukatili mara 300 Wapalestina.
Taarifa ya ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inayohusiana na jinai na
ukatili wa wanajeshi na walowezi wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina
imeongeza kuwa, katika mwaka 2013 wanajeshi wa Israel wameshambulia
maeneo mbalimbali ya Palestina na kuua makumi ya Wapalestina na
kuwajeruhiwa wengine 3,753.
Fauka ya hayo, walowezi wa Kizayuni nao
wamengoa zaidi ya miti elfu 10 ya mizaituni ya Wapalestina katika muda
huo kitendo ambacho takwimu zinaonesha kuwa kimeongezeka mara 25
ikilinganishwa na mwaka uliopita yaani 2012. Kabla ya hapo pia Baraza
Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha kwa wingi wa kura haki ya
Wapalestina ya kumiliki ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni
tangu mwaka 1967 ukiwemo mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas, jambo aambalo
ni tangazo jengine la jamii ya kimataifa kwamba inapinga ujenzi wa
vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina. Hii ni
katika hali ambayo, mazungumzo ya mapatano kati ya Mamlaka ya Ndani ya
Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel yaliyokuwa yamekwama kwa muda
wa miaka mitatu yalianza tena mwezi Julai mwaka huu kwa mashinikizo ya
Marekani kwa Wapalestina na kuendelea hadi siku chache zilizopita.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa viongozi wa utawala wa Kizayuni katika
kipindi chote hiki cha mazungumzo yanayokwama na kukwamuka kati ya
Mamlaka ya Ndani ya Palestina na Wazayuni, viongozi wa Israel siku zote
wamekuwa wakipoteza muda tu, hawajawahi kuheshimu hata mara moja
mazungumzo hayo na daima wamekuwa wakiendeleza siasa zao za wizi na
kupora mali za Wapalestina. Kwa maneno mengine ni kuwa, serikali
mbalimbali za utawala wa Kizayuni katika kipindi chote hiki cha miaka 20
ya mazungumzo na Wapalestina, zimekuwa zikijionesha kwamba zinapenda
amani, lakini kila leo Wazayuni wanafanya jinai dhidi ya Wapalestina,
wanapora ardhi zao, wanavunja makazi yao, wanaharibu mashamba yao na
wanawashambulia kikatili kwa kila aina ya silaha, huku wakiwazingira
kila upande Wapalestina hao madhlumu. Saib Uraiqat, mkuu wa timu ya
Mamlaka ya Ndani ya Palestina inayofanya mazungumzo ya mapatano na
Wazayuni amesema kuwa, mazungumzo ya moja kwa moja ya mapatano kati ya
mamlaka hiyo na Wazayuni kwa upatanishi wa Marekani yamekwama muda mrefu
nyuma na kwamba kinachofanyika hivi sasa ni mazungumzo kati ya
Wapalestina na Wamarekani kwa upande mmoja, na Wamarekani na Wazayuni
kwa upande wa pili. Jambo hilo nalo lina maana ya kwamba siasa za miaka
20 sasa za Mamlaka ya Ndani ya Palestina za kufanya mazungumzo na
Wazayuni zimefeli kikamilifu na zimekuwa ni kwa madhara ya Wapalestina.
Ni kwa sababu hiyo ndio maana wachambuzi wa mambo wakasema kuwa, msimamo
wa makundi ya muqawama ya Palestina kwamba utawala wa Kizayuni hauelewi
lugha yoyote isipokuwa mtutu wa bunduki, ndio uliowaletea manufaa
Wapalestina na si siasa za kukubali kuburuzwa kwenye mazungumzo yenye
madhara makubwa kwa taifa la Palestina zinazoendeshwa na Mamlaka ya
Ndani ya Palestina.
No comments:
Post a Comment