Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Thursday, November 21, 2013

Nchi za Kiarabu na Kiafrika zajaribu kukabiliana na changamoto za kiusalama na kiuchumi

Kikao cha tatu cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu' Arab League' na Umoja wa Afrika 'AU' kimemalizika nchini Kuwait kwa kutiwa saini makubaliano 29 kati ya pande hizo mbili. Wakuu wa nchi za Kiarabu na Kiafrika walikutana kwa muda siku mbili nchini Kuwait, ambapo siku ya Jumatano walitoa taarifa ya pamoja na kutiwa saini makubaliano 29 katika nyanja mbalimbali, kwa lengo  la kuongeza mashirikiano kati ya pande hizo mbili. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, imepangwa kuwa kiwango cha mashirikiano ya kiistratijia kiongezwe katika masuala ya kiusalama  kati ya  pande hizo mbili.
Taarifa hiyo ya pamoja imeeleza wasiwasi wa kuwepo changamoto zinazosababisha kukosekana usalama na utulivu katika baadhi ya nchi, na kusisitiza juu ya udharura wa kubadilishana taarifa za kiusalama kwa lengo la kukabiliana na makundi ya kigaidi. Taarifa hiyo imezitaka nchi za Kiarabu na Kiafrika zifanye juhudi kubwa za kutatua migogoro ya kisiasa katika maeneo yao. Hivi sasa nchi za Kiarabu na Kiafrika zinakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile changamoto za kiuchumi, kisiasa na kiusalama. Hali kadhalika imeelezwa kuwa, masuala mbalimbali ya kimsingi yanaonekana kuwa na nafasi ya kuibuka changamoto hizo. Taarifa hiyo imeeleza kuwa, masuala mbalimbali ya kimsingi ya ndani na ya kigeni katika miaka ya hivi karibuni, yamezidisha matatizo ya kiuchumi na kiusalama kwa nchi hizo. Taarifa hiyo ya nchi za Kiarabu na Kiafrika imeeleza kuwa, moja ya changamoto muhimu inayozikumba nchi hizo, ni kutozingatiwa masuala mbalimbali ya kimsingi ya ndani na kieneo. Nafasi muhimu na chanya ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Umoja wa Afrika, inaweza kuleta  mafanikio ya kutekelezwa  malengo ya nchi hizo. Tunapoziangalia baadhi ya nchi za Kiarabu na Kiafrika nje ya taasisi hizo za kieneo, tunaona kuwa zina ushawishi na nafasi muhimu katika kupatikana changamoto za kiuchumi na kiusalama. Kwa mfano, Saudi Arabia ikiwa ni moja kati ya nchi mwanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, kutokana na ushawishi na nafasi kubwa iliyokuwa nayo nje ya jumuiya hiyo, imekuwa ikichukua misimamo ya upande mmoja, suala ambalo limechangia kuongezeka  machafuko katika eneo la kijiografia la jumuiya hiyo ya Kiarabu.
Bandar bin Sultan bin Abdulaziz Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Saudi Arabia amesababisha kushadidi  machafuko kaskazini mwa Lebanon, Syria na Iraq kutokana na uamuzi wake wa kuyaongoza makundi ya kigaidi katika eneo la Mashariki ya Kati. Hii ni katika hali ambayo, nchi wanachama wa  Arab League kwa kushirikiana na taasisi nyingine za ndani na kieneo zinaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuleta utulivu na kuondoa changamoto za kiusalama na kiuchumi katika eneo hilo. Umoja wa Afrika nao pia ukiwa na wanachama zaidi ya 50 una suhula nyingi za kiuchumi na kisiasa na kwamba ushirikiano wa nchi wanachama wa umoja huo unaweza kuondoa tatizo kubwa linalozikabili  nchi hizo, yaani changamoto ya kiuchumi. Bara la Afrika lina utajiri mkubwa wa maliasili na kama nchi hizo zitaweza kutumia kwa njia sahihi maliasili na utajiri huo katika kalibu ya mashirikiano ya kieneo na kuweka misingi imara ya kiuchumi, basi linaweza kuondoa matatizo ya kiuchumi yanayozikumba nchi za Kiafrika, kama vile Somalia na Sudan Kusini. Uzoefu wa kihistoria unaonyesha kuwa, kuimarishwa miundombinu ya kiuchumi na kutatuliwa matatizo ya kimaisha ya wananchi, ni fursa nzuri ya kuondosha changamoto zilizopo za kiusalama na kutokomeza  vitendo vya kigaidi. Bila shaka suala hilo linaweza kutekelezeka kivitendo iwapo nchi za Kiarabu na Kiafrika zitakuwa na mashirikiano ya dhati na hasa ikizingatiwa kuwa, nchi hizo zina  mitazamo ya pamoja ya kihistoria, kiutamaduni na ya kidini.   

No comments: