Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Wednesday, July 17, 2013

Zaidi ya walimu laki mbili kufutwa kazi Kenya

Tume ya Kuajiri Walimu nchini Kenya (TSC) imeanzisha mikakati ya kuajiri walimu wapya watakaochukua nafasi za wale wanaogoma. Kwa mujibu wa tume hiyo, walimu watakaopoteza nafasi zao za kazi ni wale waliokosa kurudi kazini kuambatana na agizo la mahakama lililotolewa Julai 1, na waliokataa kutii amri ya serikali iliyotolewa Jumatatu iliyopita.
Agizo la serikali lililotolewa na Waziri wa Elimu, Prof. Jacob Kaimenyi, lilisema walimu ambao wangekosa kurudi kazini Jumanne ya jana wangechukuliwa kama waliokwepa kazi na kuadhibiwa. Prof Kaimenyi alikuwa amesema TSC ina mamlaka ya kuchukua hatua dhidi ya walimu waliokosa kurudi kazini, kwa kuwa sheria inaruhusu mwajiri kumwadhibu muajiriwa wake anapokosa kuhudumu inavyostahili. Tayari TSC imewataka watu waliohitimu katika taaluma ya uwalimu watume maombi ya kazi.  Hata hivyo, mwenyekiti wa chama cha kitaifa cha walimu nchini Kenya KNUT, Bw. Wilson Sossion, amepuuzilia mbali harakati za TSC na kuitaka serikali kukoma kuwatisha walimu na badala yake iwalipe marupurupu yao. Mgomo wa walimu katika shule za umma kote nchini Kenya umeingia wiki ya 3 sasa huku zikiwa zimesalia wiki chache kabla ya muhula wa pili kumalizika.

No comments: