Leo ni Jumatano tarehe 8 Ramadhani mwaka 1434 Hijria inayosadifiana na tarehe 17 Julai 2013.
Miaka 45 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo chama cha
Baath cha Iraq kilichukua hatamu za uongozi kupitia mapinduzi
yaliyoongozwa na Ahmad Hassan al Bakr na kumpindua Rais Abdulrahman
Aarif. Baada ya kuchukua madaraka chama cha Baath, Saddam Hussein ambaye
alikuwa kiongozi nambari mbili wa chama hicho alianza kuwauwa wapinzani
wake nchini Iraq na vikosi vya usalama na vya jeshi la nchi hiyo pia
vikaanzisha hujuma kali dhidi ya Wakurdi wapinzani, wazalendo,
wanaharakati wa Kiislamu na hata Wakomonisti.
Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita Profesa Roger Garaudy,
mwanafalsafa na mwanafikra wa Ufaransa alizaliwa huko katika mji wa
Marseille. Garaudy alipata shahada ya daraja ya udaktari katika taaluma
tatu za masomo ya falsafa, fasihi na utamaduni. Roger Garaudy alifungwa
jela katika kambi ya mateka wa kivita wa Ujerumani tangu mwaka 1940 hadi
1943 kutokana na mapambano yake dhidi ya ufashisti wa Adolph Hitler
wakati Ufaransa ilipokaliwa kwa mabavu na Ujerumani. Profesa Garaudy
alikuwa mwanachama wa chama cha Kikomonisti cha Ufaransa kwa miaka 36 na
pia mwanachama wa kamati kuu ya chama hicho kwa miaka 25. Hata hivyo
mitazamo ya kikomunisti na kiliberali haikuweza kukata kiu ya kutafuta
ukweli ya msomi huyo wa Ufaransa na hatimaye alikubali dini ya tukufu ya
Kiislamu baada ya kufanya utafiti mkubwa. Ushindi wa Mapinduzi ya
Kiislamu nchini Iran mwaka 1979 ulikuwa na taathira kubwa katika
mitazamo ya Profesa Roger Garaudy.
Na tarehe 8 Ramadhani miaka 759 iliyopita alifariki dunia Najmuddin
Ali Dabiran maarufu kwa jina la Katibi ambaye alikuwa mwanafalsafa na
mnajimu mkubwa wa Kiisrani. Hakuna maandiko yanayoashiria historia ya
kipindi cha awali cha maisha ya msomi huyu lakini maisha yake yanaonesha
kuwa Khaja Nasiruddin Tusi alimtaka katibi kumsaidia katika kituo chake
cha elimu ya nujumu huko Maraghe.
Katibi ameandika vitabu kadhaa kama "Jamiud Daqaiq" na "Hikmatul Ain".
No comments:
Post a Comment