Polisi ya Marekani imeendelea kuwatia nguvuni waandamanaji wanaopinga
hukumu ya mahakama ya nchi hiyo iliyomuachia huru askari aliyemuua
Mmarekani kijana mwenye asili ya Afrika kwa kumpiga risasi bila ya hatia
yoyote. Ripota wa Press tv amesema Wamarekani waliendelea kuandamana
jana katika miji ya California na Los Angeles
wakipinga uamuzi wa
mahakama ya Florida wa kumuondoa hatiani askari wa zamu George Zimmerman
aliyemuua kijana Mmarekani-Mwafrika ambaye hakuwa na silaha yoyote
wakati anauawa.
Mjini Washington pia wapinzani wa hukumu ya mahakama hiyo
walikusanyika kwa siku ya pili mfululizo mbele ya Ikulu ya White House
kuonesha hasira zao dhidi ya uamuzi huo uliotambuliwa na wengi kuwa
umetolewa kwa misingi ya kibaguzi.
Maandamano na ghasia kubwa za kupinga ubaguzi unaofanywa na vyombo
vya usalama na mahakama za Marekani dhidi ya Wamarekani wenye asili ya
Afrika pia zimeshuhudiwa katika miji mbalimbali ya Marekani.
Machafuko hayo yalianza Jumamosi iliyopita baada ya mahakama moja ya
Florida kumuondoa hatiani mlinzi mzungu Zimmerman aliyemuua kijana
Mmarekani-Mwafrika Trayvon Martin ambaye hakuwa na silaha.
Wanaharakati wa haki za kiraia wanapanga kuitisha maandamano makubwa
katika miji mia moja ya Marekani Jumamosi ijayo kupinga ubaguzi
unaowalenga Wamarekani wenye asili ya Afrika.
No comments:
Post a Comment