Umoja wa Mataifa umesema unafikiria suala la kusitisha msaada kwa
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) baada ya kubainika
kwamba baadhi ya wanajeshi wa serikali wamekuwa wakiivunjia heshima
miili ya waasi wa M23 waliouawa vitani na kuwatesa wafungwa.
Akizungumza jana Jumatano, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Ban-Ki-moon alielezea wasi wasi wake kuhusu
vitendo hivyo vya askari wa
Kongo katika kipindi hiki cha kushadidi mapigano mashariki mwa nchi
hiyo.
Jeshi la Kongo limesema litachunguza tuhuma hizo na kuwachukulia
hatua za kisheria wahusika. Jeshi la Kongo linaendeleza mashambulizi
dhidi ya ngome za waasi wa M23 karibu na mji wa Goma na kupelekea mamia
ya wanakijiji kukimbia makaazi yao. Katika taarifa jeshi hilo la
limeeleza kuwa, limeanza kushambulia kwa makombora eneo la Kibati
lililoko umbali wa kilomita 15 kaskazini mwa Goma, makao makuu ya jimbo
la Kivu Kaskazini.
Waasi wa M23 walianza kuchukua udhibiti wa baadhi ya maeneo ya
mashariki mwa Kongo mwaka jana kwa madai kuwa serikali ya Kinshasa
haijatekeleza makubaliano ya amani ya mwaka 2009.
No comments:
Post a Comment