John Kerry Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani Jumanne usiku
alikutana na kufanya mazungumzo na Mahmoud Abbas Rais wa Serikali ya
Ndani ya Palestina huko Jordan kwa shabaha ya kuhuisha eti mazungumzo ya
amani Mashariki ya Kati. Mazungumzo hayo yamepingwa vikali na wananchi
wengi wa Palestina. Akiwa katika safari yake ya sita katika eneo la
Mashariki ya Kati baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni
wa Marekani, John Kerry
amefanya mazungumzo na Rais Mahmoud Abbas Rais
wa Serikali ya Ndani ya Palestina katika juhudi za kuurejesha utawala wa
Kizayuni na Wapalestina katika meza ya mazungumzo ya mapatano eti ya
Mashariki ya Kati.
Japokuwa hakuna taarifa iliyotolewa kuhusu mazungumzo hayo
yaliyofanyika kwa muda wa masaa matano, lakini nukta hii inapasa
kutiliwa maanani kwamba, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani
amelifanya suala la kufuatilia mchakato eti wa mapatano wa Mashariki ya
Kati kuwa moja ya vipaumbele vyake vikuu katika ajenda yake tangu
alipoteuliwa katika nafasi hiyo tarehe Mosi Februari mwaka huu.
Baada ya mazungumzo hayo ya Kerry na Abbas huko Amman nchini Jordan,
imetangazwa kuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani jana pia
alitarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi zilizounga mkono
mpango wa amani wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wa mwaka 2002. Mpango huo
unajumuisha kutambuliwa kikamilifu Israel iwapo majeshi ya utawala huo
yataondoka katika ardhi za Palestina zilizoghusubiwa mwaka 1967 na
kukubali kutatuliwa kwa uadilifu kadhia ya wakimbizi wa Kipalestina.
Mpango huo wa Arab League ambao umepingwa na Israel, unakabiliwa na
vizuizi vingi kwa kuzingatia kwamba, utawala wa Kizayuni si tu kuwa
unapinga kurejea katika mipaka ya mwaka 1967, bali pia unakataa
kurejeshewa Wapalestina eneo la Quds Mashariki na vilevile haki ya
wakimbizi wa Palestina ya kurudi katika ardhi zao ambazo hadi sasa
zinakaliwa kwa mabavu na Israel.
Ukweli ni kuwa Kerry ana matarajio ya kufufua mazungumzo eti ya
mapatano kati ya Israel na Wapalestina kwa hali yoyote ile, ambayo
yalikwama mwaka 2010 baada ya kuibuka mjadala kuhusu suala la ujenzi wa
vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Wapalestina katika
Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds Mashariki.
Duru mpya ya jitihada za Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kwa
ajili ya kufufua mchakato wa mazungumzo eti ya mapatano kati ya Israel
na Wapalestina imeanza katika hali ambayo raia na makundi mengi ya
Palestina yanaamini kuwa, mazungumzo hayo yatakuwa na madhara kwa
Wapalestina. Vilevile serikali halali ya Palestina inayoongozwa na
Hamas huko katika Ukanda wa Ghaza imetangaza kuwa lengo la safari za
mara kwa mara za viongozi wa Marekani akiwemo John Kerry na William
Bernz katika eneo la Mashariki ya Kati na katika ardhi za Palestina
zinazokaliwa kwa mabavu na Israel ni kwa ajili tu ya kupoteza muda na
kuzipotosha fikra za walio wengi ili kuficha mipango ya ujenzi wa
vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina.
Katika mazingira hayo japokuwa John Kerry Waziri wa Mashauri ya
Kigeni wa Marekani analipa kipaumbele suala la kufufua mazungumzo eti ya
mapatano kati ya Wapalestina na Israel, lakini inatabiriwa kuwa
mazungumzo hayo yatafeli hata kama Mahmoud Abbas Rais wa Mamlaka ya
Ndani ya Palestina pia atakubali kwa mara nyingine tena kushiriki katika
mazungumzo hayo na Israel.
No comments:
Post a Comment