Naibu Spika wa Baraza la Seneti la Italia Roberto Calderoli ambaye
amemfananisha Waziri wa Uhamiaji wa nchi hiyo mwenye asili ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo Cecile Kyenge kuwa ni "orangutangu" kwa maana ya
nyani mkubwa wa mwituni, amesema kuwa, hatajiuzulu kwa sababu ya
matamshi hayo.
Naibu Spika wa Baraza la Seneti la Italia amesema licha ya kwamba
ameomba radhi kutokana na matamshi hayo, lakini wanachama wengi wa chama
chake cha Northern League hawataki ajiuzulu.
Dharau na matamshi hayo ya kejeli na utovu wa adabu ya seneta wa
Italia dhidi ya waziri mwenye asili ya Afrika wa nchi hiyo yamezua wimbi
kubwa la ukosoaji dhidi yake katika duru za habari na mitandao ya
kijamii. Vyama na viongozi wa kisiasa wa Italia pia wanamshinikiza
seneta Roberto Calderoli ajiuluzu.
Waziri Mkuu wa Italia Enrico Letta ameyataja matamshi hayo ya dharau
ya Naibu Spika wa Baraza la Seneti la nchi hiyo dhidi ya waziri wa
serikali yake kuwa ni doa jeusi katika historia ya Italia.
Cecile Kyenge ni mmoja kati ya waziri saba wa kike katika baraza la
mawaziri la serikali Letta na amekuwa akisumbuliwa kwa hujuma za
kibaguzi tangu alipochaguliwa kuchukua nafasi hiyo. Wapinzani wake
hususan vyama vyenye misimamo mikali vya mrengo wa kulia, wamekuwa
wakimtaka aondoke katika baraza la mawaziri la Italia. Hata hivyo Bi
Kyenge amekuwa akisisitiza kuwa, anaona fakhari kuwa Mwafrika mweusi.
Cecile Kyenge ambaye alichaguliwa kuwa Waziri wa Uhamiaji wa Italia
Aprili mwaka huu, amekuwa akifanya jitihada kubwa za koboresha hali ya
wahajiri na wahamiaji nchini humo. Waziri huyo Mwafrika ana lengo la
kuwasilisha muswada ambao utawatambua watoto wa wahamiaji wanaoishi
nchini Italia kuwa ni raia wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa sheria za sasa
watoto wa wahajiri wa kigeni wanaozaliwa nchini Italia hawahesabiwi kuwa
raia wa nchi hiyo na wanaweza kuomba uraia baada ya kukamilisha miaka
18. Kwa sababu hivyo vyama vyenye misimamo mikali ya kibaguzi vya mrengo
wa kulia hususan kile kinachopiga vita wahajiri cha Northern League,
vinapinga vikali sera za waziri Kyenge.
Seneta Calderoli ambaye ni kiongozi wa chama hicho cha Northern
League, anasema sera za Waziri Cecile Kyenge zinawahamasisha wahajiri
haramu kuingia nchini Italia.
Italia ni moja kati ya nchi zinazokusudiwa na wahajiri wa Kiafrika na
inatumiwa na wahajiri hao kama lango la kuingilia katika nchi nyingine
za Ulaya. Wahajiri hao hufanya kazi dunia na kwa ujira wa chini katika
nchi nyingi za Ulaya.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa matamshi ya Seneta Calderoli ambaye
aliwahi kuwa waziri katika serikeli ya waziri mkuu aliyepita Silvio
Berlusconi, yatawachochea Wataliano wenye misimamo mikali ya kibaguzi na
kuzidisha mashambulizi ya kinyama dhidi ya wageni nchini Italia.
Hususan ikizingatiwa kwamba kwa sasa Italia inasumbuliwa na matatizo
makubwa ya kiuchumi. Deni la nchi hiyo pia limefikia yuro trilioni 3 na
kiwango cha watu wasio na ajira kimeongezeka na kufikia asilimia 26.
No comments:
Post a Comment