Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon amesema kuwa, mrengo wa
Machi 14 umekuwa ukichelewesha uundwaji wa serikali mpya nchini humo.
Baada ya kupita miezi minne ya pengo la kisiasa nchini Lebanon udharura
wa kuharakisha uundaji wa serikali nchini humo umeongezeka maradufu hasa
kwa kutilia maanani anga ya ndani iliyotanda katika nchi hiyo.
Viongozi
wa Lebanon wanasema kuwa, kutoundwa serikali mpya nchini humo ni jambo
ambalo linaipeleka nchi hiyo upande wa mgogoro na ukosefu wa amani.
Licha ya kupita miezi miwili tangu Tamman Salam alipoteuliwa kuwa
Waziri Mkuu wa Lebanon na kutakiwa aunde baraza jipya la mawaziri,
lakini ukorofi wa kisiasa na ukwamishaji mambo unaofanywa na mrengo wa
Kimagharibi wa Machi 14 unaoongozwa na Saad Hariri umekwamisha hadi sasa
kuundwa serikali nchini humo. Ukwamishaji huo wa mambo umekuwa dhahir
shahir kiasi kwamba, Nabih Berri Spika wa Bunge la Lebanon amesema
kinagaubaga kwamba, mrengo wa Machi 14 wa akina Hariri ndio unaokwamisha
kuundwa serikali kutokana na kutoa masharti ya ajabu ajabu na
yasiyotekelezeka likiwemo la kutoshirikiswa Hizbullah katika serikali
hiyo.
Michel Aoun, Mkuu wa chama cha kikristo cha Free Patriotic Movement
amesema kuhusiana na mchakato wa Waziri Mkuu Tammam Salam wa kuunda
serikali mpya kwamba, endapo Hizbullah itatupwa nje ya ulingo wa
serikali ijayo, basi chama chake pia hakitoshiriki katika serikali hiyo.
Tammam Salam aliteuliwa Aprili 6 mwaka huu kwa kura 124 za ndio huku
Wabunge wa nne tu wakijizuia kupiga kura. Baada ya uteuzi huo, Waziri
Mkuu huyo aliyechukua nafasi ya Najib mikati aliyejiuzulu alitakiwa
kuunda mara moja baraza la mawaziri. Lakini hadi sasa Tammam Salam
hajafanikiwa kuunda serikali hiyo. Tammam Salam, mwenye umri wa miaka 67
na ambaye anaungwa mkono na mrengo wa 14 ametoa pendekezo la kuundwa
"Serikali ya Maslahi ya Kitaifa" ili makundi yote ya kisiasa yaweze
kushirikishwa katika serikali hiyo. Kwa hakika akthari ya shakhsia wa
Kilebanoni wanaamini kwamba, mwafaka wa wanasiasa wa Lebanon pekee ndio
utakaoweza kukabiliana na njama na uvamizi kutoka nje ya nchi na
kuivusha salama nchi hiyo katika kipindi hiki cha mivutano ya kuunda
serikali.
No comments:
Post a Comment