Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Tuesday, June 18, 2013

Wafuasi na wapinzani wa Rais Mursi wapigana tena

Mapigano kati ya wafuasi na wapinzani wa Rais Mohammad Morsi wa Misri yameendelea kushuhudiwa kwa siku ya pili mfululizo leo mkoani al Fayoum. Mapigano hayo yalizuka baada ya mamia ya wapinzani kukusanyika mbele ya ofisi ya mkuu wa mkoa wa mji huo kufuatia wito uliotolewa na vyama na makundi mbalimbali ya kisiasa kulaani kuchaguliwa mkuu huyo wa mkoa anayetoka Harakati Ikhwanul Muslimiin. Ripoti zinasema kuwa, mkusanyiko huo ulisababisha kuzuka mapigano makali baada ya wafuasi wa rais huyo kuwashambulia waandamanaji hao na hivyo kusababisha makumi ya watu kujeruhiwa.
Hii ni katika hali ambayo juzi pia mkoa huo ulishuhudia mapigano kati ya wafanya maandamano wa Harakati ya Ikhwanul Muslimiin kwa kushirikiana na wafuasi wa chama tawala cha Uhuru na Uadilifu nchini Misri na wapinzani wanaotaka kuung’oa madarakani utawala wa Rais Morsi. Hivi karibuni Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri ilitangaza kuwa, jukumu kuu la vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo ni kulinda na kudhaminia usalama wa maeneo nyeti ya serikali na kwamba, jeshi hilo halitaingilia mgogoro wowote wa kisiasa nchini humo.

No comments: