Makamu wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar atatembelea mji mkuu
wa Sudan, Khartoum wiki ijayo. Shirika la Habari la Sudan SUNA limesema
Machar atafanya ziara hiyo wiki ijayo baada ya safari iliyokuwa
imepangwa Jumapili wiki hii kuakhirishwa kwa sababu baadhi ya mawaziri
wa Sudan walikuwa nje ya nchi. Serikali ya Sudan Kusini awali ilikuwa
imetangaza kuwa Machar ataenda Khartoum kujaribu kutatua mgogoro wa
mafuta baina ya nchi mbili.
Uhusiano wa pande mbili hizo ulizorota mwezi huu pale Sudan iliposema
itazuia mafuta ya Sudan Kusini kupita katika ardhi yake iwapo wakuu wa
Juba hawatasitisha uungaji mkono wao kwa waasi wanaoipinga serikali ya
Khartoum. Sudan Kusini inategemea mabomba ya Sudan kuuza mafuta yake
katika masoko ya kimataifa.
Mashirika ya mafuta ya China, India na Malaysia ambayo hununua mafuta
ya Sudan Kusini yanapata hasara kubwa kutokana na mzozo baina ya nchi
hizo mbili.
No comments:
Post a Comment