Sambamba na kutimia miaka 46 ya kukaliwa kwa mabavu Baitul Muqaddas,
Wapalestina na wanaharakati wanaounga mkono taifa la Palestina wamefanya
maandamano ya kupinga uzayuni katika nchi tofuati duniani na kulaani
kukaliwa kwa mabavu Quds Tukufu na kuuyahudishwa mji huo. Jana Ijumaa
Juni 7 mwaka 2013 ilisadifiana na kutimia miaka 46 ya kukaliwa kwa
mabavu Baitul Muqaddas. Baada ya kughusubu eneo la magharibi mwa Quds
mwaka 1948, jeshi la Israel mwaka 1967 pia lilikalia kwa mabavu upande
wa mashariki na kuudhibiti kikamilifu mji huo mtukufu.
Kwa mnasaba huo,
waandamanaji katika nchi 50 duniani wamelaani hatua hiyo ya Israel na
kutaka kukombolewa mji huo na wakaazi wake. Jana wanaanchi wa Misri
baada ya swala ya Ijumaa walifanya maandamano makubwa ya kupinga uzayuni
katika mji mkuu Cairo, na kuunga mkono taifa la Palestina na kuonyesha
mshikamano kwa kadhia ya Quds. Rais Muhammad Mursi wa Misri alisema
serikali yake na wananchi sanjari na kulaani jinai za utawala wa
Kizayuni, wanaunga mkono kadhia ya Palestina na maslahi ya Wapalestina
na kuendelea kufanya jitihada katika uwanja huo. Naye Ahmad Aref msemaji
wa kundi la Ikhwanul Muslimin la Misri pia amekosoa jinai na hatua za
kibaguzi za Israel dhidi ya Quds, Wapalestina na matukufu yao na kusema
kwamba lengo la maandamano hayo ni kuizindua jamii ya kimataifa
kuhusiana na suala la Quds, ili paandaliwe mazingira ya kupatikana amani
na usalama katika eneo na dunia. Nchini Mauritania pia wananchi
walifanya maandamano ya kupinga uzayuni katika mji mkuu Nouakchott na
kuzitaka nchi za Kiarabu na Kiislamu kufanya jitihada hai za kuirejesha
Quds kwa wamiliki wake wa asili, kuwafukuza wavamizi na kukomboa mji huo
mtukufu. Vilevile maelefu ya wananchi wa Jordan waliandamana jana kwa
mnasaba wa kukumbuka kutimia miaka 46 tangu mji wa Baitul Muqaddas
ukaliwe kwa mabavu. Kuhusiana na hilo pia Rais Muhammad Wahid wa
Maldives jana alipokutana na maafisa wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina
huko Ramallah alisema kuwa, msikiti wa al Aqswa ambao ni eneo takatifu
siku zote unapaswa kulindwa ili kuzuia kuvunjiwa heshima. Maelfu ya
Wapalestina pia sambamba na kufanya maandamano ya kulaani utawala wa
Kizayuni katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi
wa Mto Jordan walisisitiza kukombolewa mji wa Baitul Muqaddas na msikiti
wa al Aqswa kutoka kwa Wazayuni maghasibu. Lakini askari wa Israel
waliwashambulia kwa risasi waandamanaji hao katika Ukingo wa Magharibi
wa Mto Jordan ambapo baadhi yao walijeruhiwa. Ismail Haniya Waziri Mkuu
wa serikali halali ya Palestina amesema, kadhia ya Palestina ni kadhia
ya Kiislamu na kwamba kamwe Wapalestina hawatofumbia macho haki zao
zisizopingika kama vile Quds Tukufu na haki ya kurejea wakimbizi wa
Kipalestina katika miji na vijiji vyao. Ahmad Abu Jalibah Mkuu wa Kamati
ya Quds katika Bunge la Palestina alisisitiza mbele ya waandamanaji wa
Ukanda wa Gaza ulazima wa kuimarishwa umoja miongoni mwao ili kukomboa
Quds Tukufu kutoka kwa Israel. Maandamano kama hayo pia yamefanyika
nchini Uturuki katika miji ya Istanbul na Ankara na pia mjini London
Uingereza. Maandamano ya London yalihudhuriwa na baadhi ya wawakilishi
wa Bunge la Uingereza, Balozi wa Palestina mjini London na baadhi ya
wawakilishi wa taasisi za kisiasa, kiraia na harakati za wanafunzi na
wanawake. Utawala wa Kizayuni baada ya kuukalia kikamilifu mji wa Baitul
Muqaddas kwa kukiuka maazimio nambari 181, 194 na 242 ya Umoja wa
Mataifa, unakusudia kuuyahudisha kabisa mji huo mtukufu, kwa kujenga
huko vitongoji vya walowezi wa Kizayuni pamoja na kuwashambulia na
kuwafukuza Wapalestina.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment