Leo ni Jumatano tarehe 17 Shaaban 1434 Hijria inayosadifiana na tarehe 26 Juni 2013.
Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita Madagascar ilipata uhuru kutoka
kwa mkoloni Mfaransa. Kuanzia katikati mwa karne ya 18, Uingereza na
Ufaransa zilianzisha ushindani wa kuidhibiti nchi hiyo ya Kiafrika.
suala hilo lilipelekea kudhibitiwa mara kadhaa kisiwa hicho na nchi
mbili hizo na hatimaye mwishoni mwa karne ya 19, Ufaransa ikafanikiwa
kuidhibiti kikamilifu Madagascar.
Hata hivyo wananchi wa Madagascar
waliendesha mapambano mengi ya ukombozi dhidi ya wakoloni wa Kifaransa,
miongoni mwake ni yale ya mwaka 1947 ambapo karibu watu elfu 80
waliuawa.
Miaka 68 iliyopita sawa na tarehe 26 Juni 1945, mkutano wa kimataifa
wa San Francisco ulimaliza shughuli zake katika mji unaojulikana kwa
jina hilo huko Marekani kwa kupasishwa hati ya Umoja wa Mataifa. Mkutano
huo ambao ulikuwa wa kwanza wa kimataifa kufanyika baada ya Vita vya
Pili vya Dunia, ulihudhuriwa na wawakilishi wa nchi 50 waitifaki katika
vita hivyo.
Na siku kama ya leo miaka 759 iliyopita alizaliwa Marco Polo
mfanyabiashara na mtalii mashuhuri wa Kiitalia huko katika mji wa
Venice. Baba na mjomba wa Marco Polo walikuwa miongoni mwa watalii
mashuhuri wa Italia ambao walifanya safari huko Uchina ya Kaskazini,
Mongolia, Turkistan ya Mashariki na Iran, nchi ambazo wakati huo
zilikuwa chini ya utawala wa warithi wa Chengiz. Akiwa kijana, Marco
Polo alielekea Uchina pamoja na baba yake na kuanza kufanya biashara
nchini humo kwenye visiwa vya mashariki mwa bara la Asia kwa muda
fulani.
No comments:
Post a Comment