Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Friday, June 21, 2013

Ijumaa Juni 21 2013

Leo ni Ijumaa tarehe 12 Shaaban mwaka 1434 Hijria sawa na tarehe 21 Juni 2013 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita sawa na tarehe 31 Khordad 1360 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Dakta Mustafa Chamran, msomi na kamanda shujaa wa vikosi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Dakta Chamran alifanikiwa kupata shahada katika fani ya elektroniki na kisha akaelekea Marekani ambako alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu yaani PhD. Kwa miaka kadhaa Dakta Chamran alikuwa nchini Lebanon kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo waliokuwa wakipambana na utawala wa Kizayuni wa Israel. Mara baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Dakta Chamran alichaguliwa kuwa Waziri wa Ulinzi wa Iran na kisha akawa mbunge wa Tehran. Baada ya kuanza mashambulizi ya Iraq dhidi ya Iran, dakta Chamran alijiunga na wanapambano na kuongoza operesheni nyingi katika vita hivyo.
Sambamba na kushiriki katika mstari wa mbele vitani, Chamran alikuwa malenga na arif na ameacha maandishi mengi. Hatimaye aliuawa shahidi akiwa vitani na baada ya kufikia daraja hiyo ya juu Imam Khomeini MA alitoa ujumbe maalumu na kusema alikuwa shakhsia mwenye ikhlasi na aliyejitolea katika Jihadi kwa akili ya Allah SWT.
Miaka 43 iliyopita katika siku kma ya leo inayosadifiana na tarehe 21 Juni 1970, alifariki dunia Dakta Ahmed Sukarno kiongozi wa mapambano ya kupigania uhuru wa Indonesia. Sukarno alizaliwa mwaka 1901, na alikuwa mstari wa mbele katika mapambano yake dhidi ya mkoloni Mholanzi nchini humo. Kwa minajili hiyo, Sukarno aliwahi kukamatwa na kufungwa jela kwa miaka minne na utawala wa kikoloni wa Uholanzi. Baada ya kifungo hicho aliwahi kutiwa tena mbaroni na kubaidishwa. Mnamo mwaka 1949 alichaguliwa kuwa Rais wa Indonesia na ilipofika mwaka 1965 Ahmed Sukarno akaondolewa madarakani baada ya kufanyika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali Suharto.
Na siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, inayosadifiana na 31 Khordad 1369 Hijria Shamsia, mikoa ya Gilan na Zanjan iliyoko kaskazini na kaskazini magharibi mwa Iran ilikumbwa na mtetemeko mkubwa wa ardhi uliosababisha maafa makubwa. Zaidi ya watu elfu hamsini walifariki dunia, wengine zaidi ya elfu sitini kujeruhiwa na laki tano kukosa makaazi. Mtetemeko huo licha ya kuleta maafa kwa binadamu, ulisababisha hasara kubwa ya kiuchumi kwa wananchi na serikali.

No comments: