Mahakama ya mji wa Milan nchini Italia imemuhukumu kifungo cha
miaka saba jela, Silvio Berlusconi Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo.
Berlusconi ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Italia kwa vipindi vitatu
tofauti, alipatikana na hatia ya kujihusisha na vitendo vya ngono na
mabinti walio na umri wa chini ya miaka 18. Mahakama hiyo pia imemfungia
Berlusconi mwenye umri wa miaka 76 kujishughulisha na masuala ya siasa
kwa maisha yake yote baada ya kukumbwa na kashfa hiyo.
Hii ni mara ya tatu kwa Waziri Mkuu wa zamani wa Italia kuhukumiwa
katika kipindi cha miezi tisa iliyopita. Mwezi Oktoba 2012 alihukumiwa
kifungo cha miaka minne jela baada ya kupatikana na hatia ya kukwepa
kodi na mwezi Disemba mwaka huohuo alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja
kwa kosa la kutumia ushahidi wa kunasa mazungumzo ya simu kinyume cha
sheria.
Mahakama ya Milan imetangaza kuwa, Berlusconi anayo haki ya kukata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa.
No comments:
Post a Comment