Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanya kikao kuhusu hali
ya watoto katika vita vya silaha, ambapo pia limepokea ripoti ya Katibu
Mkuu kuhusu watoto katika vita. Ripoti hiyo imesema, hali ilikuwa mbovu
hasa katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, wakati mizozo mipya
ilipoibuka au ile iliyopo kuenea zaidi.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa kuhusu watoto na vita vya silaha, Leila Zerrougui, amesema
kuwa, wahusika wasio wa kiserikali katika mizozo wanachangia kwa kiasi
kikubwa zaidi ukiukwaji wa haki za watoto.
Miongoni mwa nchi ambazo haki za watoto zimetajwa kukiukwa katika
ripoti hiyo ni Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Magaidi wanaopata
uungaji mkono wa madola ya kigeni nchini Syria, pia wanalaumiwa kutumia
watoto vitani. Nazo Chad na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zimesifiwa
kwa hatua zilizopiga kwa kuonyesha hamu ya kuzingatia maazimio ya Baraza
la Usalama na kuweka sheria za kuwalinda watoto katika mizozo. Naye
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Watoto katika Umoja wa
Mataifa UNICEF, Yoka Brandt, amesema, lililo muhimu zaidi katika
kukomesha ukiukwaji wa haki za watoto katika vita, ni pande zinazozozana
kutekeleza majukumu yao vizuri katika kulinda haki za watoto, na wale
wanaozikiuka kukabiliwa na mkono wa sheria.
No comments:
Post a Comment