Rais Barack Obama wa Marekani amesisitiza katika duru
yake ya pili ya urais nchini humo juu ya udiplomasia wa "mashinikizo na
vikwazo" na amempa makamu wake Jo Biden jukumu la kufuatilia kadhia ya
nyuklia ya Iran. Biden ambaye ameelekea Munich, Ujerumani kwa ajili ya
kushiriki katika kikao cha usalama, ameeleza kuwa nchi yake iko tayari
kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Iran na kwamba Washington ina
mpango ambao kwa mujibu wa madai yake unaweza ukafungua njia ya
kutatuliwa kidiplomasia kadhia ya nyuklia ya Iran. Biden amesema pia
kuwa Marekani haitairuhusu Iran kumiliki silaha za nyuklia na kwamba
mlango wa mazungumzo ya amani na Tehran hautakuwa wazi milele.
Matamshi hayo ya Joe Biden yamekaribishwa na kuungwa mkono
na viongozi wa Umoja wa Ulaya akiwemo Catherine Ashton, Mkuu wa Siasa za
Nje wa umoja huo na Guido Westewelle, Waziri wa Mambo ya Nje wa
Ujerumani. Matamshi ya kiongozi huyo wa White House yanaonesha kwamba
Marekani inaendeleza siasa zake za propaganda chafu dhidi ya Iran na
kwamba Tehran kwa mujibu wa mtazamo wa Wamagharibi, ni mtuhumiwa mkubwa;
kwa sababu hiyo mazungumzo ya aina yoyote ile na Iran yanapaswa
kufanyika kwa mujibu wa madai hayo yasiyo na msingi.
Kwa hakika hatua hiyo ya Marekani ina lengo la
kuidhihirisha serikali ya Washington kuwa ina nia njema ya kutaka
kutatua kadhia ya nyuklia ya Iran kwa njia za kidiplomasia.
Ukweli wa mambo ni kuwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa
Israel zimepanga njama kabambe na harakati kubwa kwa ajili ya kikao cha
Munich na zinafanya juhudi ili kunufaika na fursa hiyo dhidi ya miradi
ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Iran. Ni kwa sababu hiyo ndio maana
katika hotuba yake kwenye mkutano wa Munich, Makamu wa Rais wa Marekani
amefanya jitihada kubwa za kuchafua sura ya Iran badala ya kuzungumzia
haki za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu.
Hii ni katika hali ambayo viongozi wa Iran wamekosoa vikali
suala la kubadilishwa mahali na tarehe ya kufanyika mazungumzo kati ya
Tehran na kundi la 5+1 na hatua ya nchi za Magharibi ya kuchapisha
habari za uwongo kuhusiana na suala hilo. Tangu karibu miezi 8 iliyopita
yaani tangu baada ya kikao cha Moscow, Iran ilikuwa imejiandaa kufanya
duru mpya ya mazungumzo, lakini upande wa Magharibi umekataa kuketi
kwenye meza ya mazungumzo kwa sababu ambazo Iran pia haizijui.
Suala kuu hapa si wakati wa kufanyika mazungumzo hayo wala
mahala gani yatafanyika, bali ni jambo jingine ambalo ni kuwa, baadhi ya
wanachama wa kundi la 5+1 hawako tayari kufanya mazungumzo hayo.
Viongozi wa Marekani wameelewa kuwa Russia na China hazichezi tena
katika uwanja wa udiplomasia wa Magharibi kama ilivyokuwa huko nyuma na
migongano ya mitazamo ya Kremlin na Peking na ile ya Marekani imepanuka
na kugusa masuala mengi kuanzia mgogoro wa Syria hadi kadhia ya nyuklia
ya Iran. Kwa sababu hiyo maafisa wa serikali ya Marekani wametoa fikra
ya kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja na Iran. Hatua hiyo
imechukuliwa kwa sababu kadhaa.
Kwanza ni kuwa Marekani na baadhi ya waitifaki wake wa
Ulaya walitarajia kuwa vikwazo vyao dhidi ya Iran vitazusha uasi na
machafuko ya kijamii. Hata hivyo badala ya kuwafanya wananchi wa Iran
waichukie serikali na mfumo wao, vikwazo hivyo vimewafanya wazichukie
zaidi nchi za Magharibi.
Sababu ya pili ni kuwa tofauti na makelele yake ya
kipropaganda, Marekani haijaweza kubuni stratijia ya maana kwa ajili ya
kuanza mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ni kwa sababu
tunapotazama mwenendo wa Marekani kuhusu Iran tutatambua kuwa madai ya
kutaka kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Tehran hayana maana
yoyote.
Ukweli ni kuwa lengo la Marekani katika harakati yake hiyo
ni kutaka kubadili mlingano wa kimataifa kuhusu suala la mazungumzo na
Iran. Duru za kisiasa za nchi za Magharibi pia zinatumia propaganda za
vyombo vya habari kuonesha kuwa Iran haiko tayari kufanya mazungumzo na
kwa njia hiyo itambulike kuwa ni tishio kwa jamii ya kimataifa.
No comments:
Post a Comment