Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Saturday, January 26, 2013

Machafuko Mtwara, Morogoro, Mahakama yachomwa moto

Askari wa jeshi la Polisi mkoani Mtwara nchini Tanzania wamelazimika kupiga mabomu ya machozi kutwa nzima hapo jana katika kata ya Chikongola, Manispaa ya Mtwara Mikindani kutawanya wananchi walioizingira nyumba ya diwani wa kata hiyo Mohamedi Chehako kwa madai ya kuwahifadhi wachawi ndani ya nyumba yake, huku mwandishi wa habari mmoja akiripotiwa kujeruhiwa. Habari ambazo hazijathibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Maria Nzuki zinadai kuwa majira ya saa 10 kasoro za jioni watu wanaodaiwa kuwa ni wanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliingilia kati na kuanza kutembeza mkong'oto kwa wananchi ili kuzima vuguvugu hilo.
Aidha wananchi hao waliokuwa na hasira  walichoma moto mahakama ya Mwanzo na kuvunja vioo vya nyumba za waheshimiwa Hawa AbdulRahman Ghasia  Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) na ya Mohamed Said Sinani  Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara. Wakiwa katika mahakama ya mwanzo, Polisi walizingirwa na vijana waliokuwa wamebeba mawe na kufunga barabara zote za kuingia na kutoka Kituo Kikuu cha Mabasi na eneo la Soko Kuu, licha ya kufyatua hewani mabomu ya machozi. Mkoa wa Mtwara katika wiki za hivi karibuni umeshuhudia maandamano na mapigano kati ya wananchi na jeshi la Polisi, kutokana na msimamo wa wananchi kupinga uamuzi wa serikali wa kutaka kuisafirisha gesi asilia kutoka mkoani humo na kuipeleka Dar es Salaam kwa njia ya mabomba. Kwa upande mwengine, vurugu kubwa zimezuka katika eneo la Dumila mkoani  Morogoro ambapo wananchi wamechoma moto nyumba na kupasua vioo vya magari  na hivyo kuzuia magari yote yanayotumia barabara hiyo, kwa madai kuwa wanapinga agizo la Mkuu wa Wilaya hiyo la kuwanyang'anya ardhi Wakulima na badala yake wamepewa Wafugaji. Vurugu hizo zimesababisha kifo cha mtu mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa.

No comments: