Maafisa wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya wameahidi kuwasaidia
wahanga wa mgogoro uliosahaulika huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. Valerie
Amos Naibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Masuala ya
Kibinadamu na ambaye pia ni Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja huo
na Kristalina Georgieva Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na
Ushirikiano wa Kimataifa ambao wako katika ziara ya siku mbili huko
Jamhuri ya Afrika ya Kati jana walitembelea mji wa Kaga Bandoro umbali
wa kilomita 350 kaskazini mwa Bangui mji mkuu wa nchi hiyo.
Wakiwa
ziarani Kaga Bandoro, maafisa hao wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya
walizungumza na wenyeji na maafisa wa mji huo na kuwaeleza kuwa hali
inayowakabili sasa haitakuwa tena mgogoro uliosahaulika. Wamesema wako
ziarani mjini humo ili kujua matatizo yao na kuifanya jamii ya kimataifa
izingatie mgogoro unaowakabili. Shule, ofisi za serikali na majego ya
Umoja wa Mataifa katika mji huo yamekabiliwa na vitendo vya uporaji mara
kadhaa tangu waasi wa Muungano wa Seleka wachukue madaraka mwezi Machi
mwaka huu. Mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi yenye silaha katika
mji wa Kago Bandoro huko Jamhuri ya Afrika ya Kati yamewapelekea wakazi
wengi wa mji huo kuishi katika misitu ya jirani na kuishi kwa kutegemea
mizizi pamoja na majani ya miti ya mihogo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment