Mkutano wa 26 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ulimaliza
shughuli zake jana usiku hapa mjini Tehran. Mkutano huo ulifanyika kwa
kaulimbiu ya "Mtume Mtukufu, Nembo ya Utambulisho wa Umma wa Kiislamu"
na umewashirikisha wanafikra na wasomi wa Kiislamu kutoka nchi 102.
Taarifa iliyotolewa na wasomi wa Kiislamu wa madhehebu mbalimbali
mwishoni mwa mkutano huo imesisitiza juu ya udharura wa kubuniwa njia za
kimatendo za kuyakurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu. Washiriki
katika mkutano huo wa kimataifa wamesema kuwa kukurubisha pamoja wafuasi
wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu ndio njia muhimu zaidi ya kufikiwa
umoja wa Umma wa Kiislamu na kusisitiza kuwa, Umma wa Kiislamu unapaswa
kushikamana na kuwa na umoja kwa shabaha ya kukabiliana na njama za
maadui.
Taarifa ya washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu
imeashiria kuwa Qur'ani Tukufu na Suna za Mtume (saw) vinamtayarishia
mwanadamu anga nzuri ya kufikia ustaarabu na ufanisi na kutilia mkazo
udharura wa kutumiwa vyema utajiri huo wa Waislamu katika maisha yao.
Mkutano wa 26 wa Umoja wa Kiislamu umeyatambua mapambano ya wananchi
wa Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel kuwa ni haki yao ya
kisheria na umezitaka jumuiya za kimataifa kuufikisha mahakamani utawala
huo kwa tuhuma ya kutenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu.
Taarifa ya washiriki katika mkutano huo pia imelaani ujenzi wa vitongoji
vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina na kutoa wito wa
kuundwa nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa Baitul Muqaddas.
Washiriki pia wamelaani mashambulizi ya kigaidi yanayofanyika katika
maeneo mbalimbali ya dunia na kusema kuwa, Uislamu unapinga ugaidi
katika sura zake zote.
Wamesisitiza pia juu ya umuhimu wa kubuniwa ufumbuzi wa Kiislamu kwa
ajili ya migogoro ya ulimwengu wa Kiislamu hususan mgogoro wa sasa wa
Syria.
Kabla ya kusomwa taarifa ya mwisho wa Mkutano wa 26 wa Kimataifa wa
Umoja wa Kiislamu, Spika wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Dakta Ali
Larijani alihutubia mkutano huo akisisitiza juu ya umuhimu wa kuwepo
umoja na mshikamano kati ya Waislamu kwa ajili ya kukabiliana na njama
za mabeberu. Dakta Larijani amesema kuwa Marekani na nchi za Magharibi
zinafanya mikakati ya kuzigawa nchi za Kiislamu na kuongeza kuwa,
udhibiti bandia wa Marekani na Magharibi umeporomoka na sasa Waislamu
wameanza kupiga hatua za maendeleo. Amesema Umma wa Kiislamu umo katika
harakati za kutengeneza historia mpya ya dunia.
Vilevile mshauri wa rais wa Sudan Abdur Rahiim bin Ali amesema katika
mkutano huo kwamba, kuna udharura wa kuimarishwa umoja na mshikamano wa
Waislamu katika mambo yanayowakutanisha wafuasi wa madhehebu zote kwa
shabaha ya kuzima njama za maadui wa Uislamu.
Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ni miongoni mwa matukio
makubwa ya ulimwengu wa Kiislamu na hufanyika kila mwaka hapa nchini
ukiwakutanisha wasomi, wanafikra na maulamaa wa madhehebu mbalimbali za
Kiislamu kwa lengo la kuimarisha umoja na mshikamano kati ya wafuasi wa
madhehebu hizo mbele ya njama na mikakati ya maadui wa umma.
No comments:
Post a Comment