Vurugu na mapigano baina ya vikosi vya usalama na waandamanaji
yameendelea kushuhudiwa katika baadhi ya miji ya Misri kwa siku ya tatu
mtawalia. Habari kutoka Misri zinasema kuwa, miji kadhaa ya nchi hiyo
ikiwemo ya Sharqia, Suez, Ismailia, Port Said na Cairo imeendelea
kushuhudia machafuko. Hali katika mji wa Port Said inaonekana kuwa mbaya
zaidi ambapo jana watu wengine saba walifariki dunia katika vurugu
zilizougubika mji huo, vurugu ambazo zilishadidi zaidi baada ya Mahakama
ya Jinai ya Misri kutoa hukumu ya kifo siku ya Jumamosi kwa watu 21
waliopatikana na hatia ya kushiriki katika ghasia za Februari mwaka jana
zilizotokea kwenye uwanja wa mpira wa miguu baada ya mechi
iliyozikutanisha klabu mbili za al Ahly na al Masry katika mji wa Port
Said. Watu wasiopungua 72 waliuawa katika ghasia hizo. Wakati huo huo
Rais Muhammad Mursi wa Misri ametangaza hali ya hatari katika miji
mitatu ya Port Said, Suez na Ismailia. Akizungumza kupitia televisheni,
Mursi amesema, hali hiyo ya hatari iliyoanza jana katika miji hiyo
itadumu kwa muda wa siku thelathini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment