Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Sunday, May 20, 2012

Wafanyamapinduzi wa Madagascar wasema wako tayari kwa maridhiano ya kitaifa

Rais wa serikali ya mpito ya Madagascar, Andry Rajoelina amesema kuwa yuko tayari kufanya maridhiano na kiongozi aliyempindua Machi 2009, Mark Ravalomanana.
Rajoelina baada ya kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amekubali kufuta uhasama ulioko kati yake na Ravalomanana hatua ambayo itaandaa mazingira bora ya kufanyika uchaguzi mkuu mpya. Weledi wa mambo wanasema kuwa tangazo la Rajoelina la kutaka maridhiano na Rais aliyepinduliwa Mark Ravalomanana ni hatua muhimu katika juhudi za kutatua mgogoro wa kisiasa nchini Madagascar.
Mgogoro huo wa kisiasa nchini Madagascar ulianza Machi mwaka 2009 wakati Andry Rajoelina akisaidiwa na baadhi ya majenerali wa kijeshi alipompindua Rais wa wakati huo Mark Ravalomanana na hivyo kumlazimisha kiongozi huyo kutangaza kujiuzulu kwake na kuikimbia nchi.
Rajoelina kipindi hicho ndiye aliyekuwa meya wa mji mkuu Antananarivo.
Punde baada ya kunyakua madaraka kupitia mapinduzi, Andry Rajoelina alianza kukabiliwa na mashinikizo kutoka kwa jumuiya za kieneo na kimataifa na mashinikizo ambayo yalimpelekea kutangaza kuwa angeandaa uchaguzi wa rais na bunge katika kipindi cha miaka miwili. Hata hivyo uchaguzi huo uliakhirishwa mwaka 2010 na 2011.
Rais wa MAdagascar : Andry Rajoelina
Tarehe ya mwisho iliyotangazwa kwa ajili ya kufanyika uchaguzi huo ni Novemba 30 mwaka huu wa 2012. Hii ni katika hali ambayo Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi nchini Madagascar imepewa hadi Mei 28 mwaka huu kuainisha tarehe ya kufanyika uchaguzi wa bunge. Tume hiyo ilibuniwa mwezi Februari mwaka huu ikiwa na dhima ya kuandaa uchaguzi wa amani, huru na wa haki nchini humo.
Hadi sasa rais wa serikali ya mpito ya Madagascar, Andry Rajoelina hajaashiria iwapo kiongozi aliyepinduliwa, Mark Ravalomanana ataruhusiwa kushiriki kwenye uchaguzi ujao wa rais au la, ingawa mara kadhaa amesisitiza kuwa yeye mwenyewe hatoshiriki kwenye uchaguzi huo kwa sharti kuwa nao marais wa zamani wa nchi hiyo pia wasishiriki. Kwa sasa Mark Ravalomanana anaishi uhamishoni nchini Afrika Kusini na wafanyamapinduzi wa Madagascar wamesema kuwa akirejea nchini anapaswa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kutokana na maandamano ya mwaka 2009 yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa. Baada ya mapinduzi ya Machi 18 mwaka 2009, Andry Rajoelina amekuwa akitumia mbinu mbalimbali kuhalalisha uongozi wake na tunaweza kusema kuwa kura ya maoni kuhusu katiba mpya iliyofanyika miaka miwili iliyopita pia ilikuwa katika fremu hiyo hiyo. Ni jambo lisilopingika kuwa baada ya mashinikizo ya muda mrefu, sasa Andry Rajoelina amekubali kuandaa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kuhitimisha mgogoro wa miaka 4 wa kisiasa nchini Madagascar.

No comments: