Sambamba na kukaribia uchaguzi wa kwanza nchini Misri baada ya ku'ngolewa madarakani dikteta Hosni Mubarak, uvumi unaongezeka kwamba Baraza Kuu la Kijeshi linalotawala nchi hiyo linafanya njama za kuingilia mwenendo wa upigaji kura na kuchakachua matokeo ya uchaguzi huo. Baraza hilo likishirikiana na wapinzani wa ndani na nje wa mapinduzi ya wananchi wa Misri siku zote limekuwa likifanya njama nyingi ili kupotosha malengo ya mapinduzi hayo.
Mwanzoni kulifanyika njama za kuzusha woga na wasiwasi miongoni mwa wananchi, mauaji, ukandamizaji mkubwa wa maandamano ili kuzuia kufanyika uchaguzi wa bunge nchini humo. Baada ya kuona msimamo madhubuti ulioonyeshwa na wananchi na kusimama kwao kidete, uchaguzi wa bunge ulifanyika katika wakati uliopangwa. Katika uchaguzi huo wagombea wa vyama vya Kiislamu walishinda viti vingi zaidi ikilinganishwa na vyama vingine vya Misri. Lakini matokeo hayo hayakukubaliwa na wapinzani wa ndani na nje wa mapinduzi wa Misri. Wakati huo huo, mkakati mwingine uliofanyika ili kupotosha na kuharibu mapinduzi ya wananchi wa Misri ni kuingilia mwenendo wa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo. Ili kufanikisha njama hiyo njia mbalimbali zimetumika, muhimu zaidi ya yote ikiwa ni kumuingiza katika uchaguzi huo jasusi mkuu wa dikteta Hosni Mubaraka Omar Suleiman na baadaye kubatilisha ugombea wake, ili kwa njia hiyo waweze pia kumtoa Khairat al Shater aliyekuwa mgombea asili wa harakati ya Ikhwanul Muslimin.
Matokeo ya uchaguzi katika vituo vya nje ya Misri ambao wagombea wa vyama vya Kiislamu wameshinda, umeonesha kuwa njama hizo hadi sasa hazijafanikiwa kuwafanya wagombea wasiotoka katika vyama vya Kiislamu washindwe. Hii ni katika hali ambayo uchunguzi wa kura za maoni pia unaonyesha kuwa, ndani ya Misri nako wanaharakati wa Kiislamu wana nafasi kubwa zaidi ya kushinda uchaguzi huo. Ukwamishaji huo wa Baraza Kuu la Kijeshi na wapinzani wa mapinduzi ya wananchi wa Misri umepelekea hivi sasa wakati uchaguzi huo wa rais ukikaribia, wanaharakati na vyama vya Kiislamu nchini humo waelewe hali ilivyokuwa nyeti hivi sasa na kuhisi hatari kwamba huenda baraza hilo la kijeshi likafanya udanganyifu na wizi wa kura katika uchaguzi huo. Sharif Jabir mjumbe wa Sekretarieti ya Masuala ya Kiutamaduni ya Chama cha Uhuru na Uadilifu cha Misri amesema anatabiri kutakuwepo wizi wa kura na udanganyifu katika uchaguzi wa rais wa Misri na kusema kuwa, katika kikao cha wiki hii cha bunge la nchi hiyo, watajadili suala hilo. Mjumbe huyo ameashiria zoezi la upigaji kura lenye kutia shaka huko NewYork Marekani wakati wa uchaguzi wa nje ya nchi na kutoruhusiwa kushuhudia tukio hilo baadhi ya waandishi habari na kusema kwamba, wana malalamiko kuhusu uingiliaji uliofanyika katika baadhi ya balozi za Misri, kwa kuwa zoezi hilo lilifanyika bila kuwepo wawakilishi wa wajumbe wa vyama husika. Suala muhimu pia ni kuhusiana na uingiliaji wa nchi za Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu katika uchaguzi wa rais wa Misri. Nchi hizo zimetoa misaada mingi ya fedha kwa wagombea kama vile Ahmad Shafiq na Amr Musa wa ndani na nje ya nchi wenye mfungamano na utawala uliopita nchini Misri, ili kuzuia wagombea wa mirengo ya Kiislamu wasishinde uchaguzi huo.
No comments:
Post a Comment