Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC yenye makao yake mjini Hague, Uholanzi, karibuni hivi itawafungulia mashtaka washukiwa wanne wa machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 nchini Kenya. Uhuru Kenyatta, William Ruto, Francis Muthaura na Joshua Sang wanatuhumiwa kuhusika kwa njia moja au nyingine katika machafuko hayo ya baada ya uchaguzi mkuu wa Rais uliofanyika Disemba mwaka 2007. Kwenye machafuko hayo yaliyoendelea hadi mwanzoni mwa mwaka 2008, takriban watu 1300 waliuawa na mamia ya maelfu ya wengine kuachwa bila makao na hivyo kulazimika kuwa wakimbizi wa ndani. Kwenye uchaguzi huo, ushindani mkali ulikuwa kati ya Raila Odinga wa chama cha ODM na Rais Mwai Kibaki wa PNU. Machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi mkuu huo yalichochewa zaidi na uhasama kati ya wafuasi wa viongozi hao wawili. Baadaye harakati za upatanishi zilizoongozwa na Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa zilizaa matunda ambapo Mwai Kibaki pamoja na Raila Odinga walikubaliana kugawana madaraka na hivyo kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa. Mwai Kibaki aliendelea kushikilia wadhifa wa Rais naye Odinga akateuliwa kuwa Waziri Mkuu. Hadi sasa juhudi zimefanywa ili kuepuka kujikariri machafuko yalishuhudiwa mwishoni mwa mwaka 2007 na mwanzoni mwa mwaka 2008 na ili kufikia lengo hilo, miaka miwili iliyopita sheria zote za uchaguzi zilibadilishwa. Uchaguzi mkuu ujao unatarajiwa kufanyika Machi 4 mwaka ujao wa 2013 na utakuwa wa kwanza kufanyika chini ya katiba mpya ya Kenya iliyopitishwa kwenye kura ya maoni mwezi Agosti mwaka 2010. Kwa mujibu wa katiba hiyo mpya, Ili mgombea urais aweze kutangazwa mshindi kwenye duru ya kwanza, atatakiwa kupata asilimia 25 ya kura zote katika majimbo yasiyopungua 24 kati ya 47 ya nchi hiyo na pia kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zitakazopigwa. Kinyume na hilo, uchaguzi utalazimika kuingia duru ya pili. Uhuru Kenyatta na William Ruto ambao ni miongoni mwa washukiwa wanne wa machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, wametangaza nia yao ya kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu ujao. Wawili hao wameungana pamoja na wanasiasa wengine ili kuimarisha upinzani dhidi ya Bw, Odinga ambaye wachambuzi wengi wanaamini kwamba anayo nafasi nzuri ya kuwa Rais wa nne wa Kenya. Ni jambo lililowazi kwamba endapo mahakama ya ICC itawafungulia Mashtaka Uhuru Kenyatta na William Ruto kabla ya uchaguzi mkuu ujao, itibari yao ya kisiasa itashuka. Wachambuzi wa mambo wanaitakidi kuwa kesi za raia wanne wa Kenya katika mahakama ya kimataifa ya Jinai ICC itakuwa mtihani mkubwa wa kupima kiwango cha ushirikiano kati ya serikali ya Kenya na mahakama hiyo.
No comments:
Post a Comment